Nahumu 1
1
1 # Taz Isa 10:5-34; 14:24-27; Sef 2:13-15 Kauli ya Mungu juu ya Ninewi. Kitabu cha maono ya Nahumu wa Elkoshi.
Ghadhabu ya Mungu dhidi ya Ninewi
2Mwenyezi-Mungu ni Mungu mwenye wivu, mlipiza kisasi;
Mwenyezi-Mungu hulipiza kisasi na ni mwenye ghadhabu;
Mwenyezi-Mungu hulipiza kisasi kwa adui zake,
huwaka ghadhabu juu ya adui zake.
3Mwenyezi-Mungu hakasiriki upesi, lakini amejaa nguvu,
Mwenyezi-Mungu kamwe hatawaachilia wenye hatia.
Apitapo Mwenyezi-Mungu, huzuka kimbunga na dhoruba;
mawingu ni vumbi litimuliwalo na nyayo zake.
4Huikaripia bahari na kuikausha,
yeye huikausha mito yote.
Mbuga za Bashani na mlima Karmeli hunyauka,
maua ya Lebanoni hudhoofika.
5Milima hutetemeka mbele yake,
navyo vilima huyeyuka;
dunia hutetemeka mbele yake,
ulimwengu na vyote vilivyomo.
6Nani awezaye kuikabili ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu?
Nani awezaye kustahimili ukali wa hasira yake?
Yeye huimwaga hasira yake iwakayo kama moto,
hata miamba huipasua vipandevipande.
7Mwenyezi-Mungu ni mwema,
yeye ni ngome ya usalama wakati wa taabu.
Yeye huwalinda wote wanaokimbilia usalama kwake.
8Adui wakiivamia nchi kama mafuriko, yeye huwaangamiza;
huwafuatia na kuwafukuza mpaka gizani.
9Mbona mnafanya mipango dhidi ya Mwenyezi-Mungu?
Yeye atawakomesha na kuwaangamiza,
wala mpinzani wake hataweza kuinuka tena.
10 # 1:10 maana ya aya hii katika Kiebrania si dhahiri. Watateketezwa kama kichaka cha miiba,
kama vile nyasi zilizokauka.
11Kwako kumetoka aliyepanga maovu dhidi ya Mwenyezi-Mungu
aliyefanya njama za ulaghai.
12Mwenyezi-Mungu awaambia hivi watu wake:
“Ingawa Waashuru ni wengi na wenye nguvu,
wao wataangushwa na kuangamizwa.
Ingawa nimewatesa nyinyi watu wangu,
sitawateseni tena zaidi.
13Sasa nitaivunja nira ya Ashuru shingoni mwenu,
na minyororo waliyowafungia nitaikatakata.”
14Mwenyezi-Mungu ameamuru hivi kuhusu Ninewi:
“Hutapata wazawa kulidumisha jina lako.
Sanamu zako za kuchonga na za kusubu,
nitazivunjavunja nyumbani mwa miungu yako.
Mimi nitakuchimbia kaburi lako,
maana wewe hufai kitu chochote.”
15 # Taz Isa 52:7 Enyi watu wa Yuda tazameni:
Anakuja kutoka mlimani mtu anayeleta habari njema,
mjumbe ambaye anatangaza amani.
Adhimisheni sikukuu zenu, enyi watu wa Yuda,
timizeni nadhiri zenu,
maana waovu hawatawavamia tena,
kwani wameangamizwa kabisa.
Iliyochaguliwa sasa
Nahumu 1: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.