Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 8:14-26

Marko 8:14-26 BHN

Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate; walikuwa na mkate mmoja tu katika mashua. Yesu akawaonya, “Angalieni sana! Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.” Wanafunzi wakaanza kujadiliana wao kwa wao, “Anasema hivyo kwa kuwa hatuna mikate.” Yesu alitambua hayo, akawaambia, “Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu ni mizito? Je, mnayo macho na hamwoni? Mnayo masikio na hamsikii? Je, hamkumbuki wakati ule nilipoimega ile mikate mitano na kuwapa watu 5,000? Mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki.” Wakamjibu, “Kumi na viwili.” “Na nilipoimega ile mikate saba na kuwapa watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki?” Wakamjibu, “Saba.” Basi, akawaambia, “Na bado hamjaelewa?” Yesu alifika Bethsaida pamoja na wanafunzi wake. Huko watu wakamletea kipofu, wakamwomba amguse. Yesu akamshika huyo kipofu mkono, akampeleka nje ya kijiji. Akamtemea mate machoni, akamwekea mikono, akamwuliza, “Je, unaweza kuona kitu?” Huyo kipofu akatazama, akasema, “Ninawaona watu wanaoonekana kama miti inayotembea.” Kisha Yesu akamwekea tena mikono machoni, naye akakaza macho, uwezo wake wa kuona ukamrudia, akaona kila kitu sawasawa. Yesu akamwambia aende zake nyumbani na kumwamuru, “Usirudi kijijini!”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Marko 8:14-26