Marko 5:21-43
Marko 5:21-43 BHN
Yesu alivukia tena upande wa pili wa ziwa kwa mashua. Umati mkubwa wa watu ukakusanyika mbele yake, naye akawa amesimama kando ya ziwa. Hapo akaja mmojawapo wa maofisa wa sunagogi aitwaye Yairo. Alipomwona Yesu, akajitupa mbele ya miguu yake, akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa karibu na kufa. Twende tafadhali, ukamwekee mikono yako, apate kupona na kuishi.” Basi, Yesu akaondoka pamoja naye. Watu wengi sana wakamfuata, wakawa wanamsonga kila upande. Mmojawapo alikuwa mwanamke mwenye ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Mwanamke huyo alikuwa amekwisha sumbuka sana kuwaendea waganga wengi. Na ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote, hakupata nafuu bali hali yake ilizidi kuwa mbaya. Alikuwa amesikia habari za Yesu, na hivyo akaupenya msongamano wa watu kutoka nyuma, akagusa vazi lake. Alifanya hivyo, maana alijisemea, “Nikigusa tu vazi lake, nitapona.” Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, akajisikia mwilini mwake kwamba ameponywa ugonjwa wake. Yesu alitambua mara kwamba nguvu imemtoka. Basi akaugeukia ule umati wa watu, akauliza, “Nani aliyegusa mavazi yangu?” Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi watu wanavyokusonga; mbona unauliza nani aliyekugusa?” Lakini Yesu akaendelea kutazama amwone huyo aliyefanya hivyo. Hapo huyo mwanamke, akifahamu yaliyompata, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa chini mbele ya Yesu na kusema ukweli wote. Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.” Yesu alipokuwa bado anaongea, watu walifika kutoka nyumbani kwa yule ofisa wa sunagogi, wakamwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Ya nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?” Lakini, bila kujali walichosema, Yesu akamwambia mkuu wa sunagogi, “Usiogope, amini tu.” Wala hakumruhusu mtu yeyote kufuatana naye ila Petro, Yakobo na Yohane nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa ofisa wa sunagogi naye Yesu akasikia makelele, kilio na maombolezo mengi. Akaingia ndani, akawaambia, “Mbona mnapiga kelele na kulia? Msichana hakufa, amelala tu.” Lakini wao wakamcheka. Basi, akawatoa wote nje, akawachukua baba yake na mama yake huyo msichana na wale wanafunzi wake, wakaingia chumbani alimokuwa huyo msichana. Kisha akamshika mkono, akamwambia, “Talitha, kumi,” maana yake, “Msichana, nakuambia, amka!” Mara msichana akasimama, akaanza kutembea. (Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.) Hapo watu wakashangaa kupita kiasi. Yesu akawakataza sana wasimjulishe mtu jambo hilo. Kisha akawaambia wampe huyo msichana chakula.