Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 12:13-27

Marko 12:13-27 BHN

Basi, baadhi ya Mafarisayo na wafuasi wa kikundi cha Herode walitumwa ili wamtege Yesu kwa maneno yake. Wakamwendea, wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu unayesema ukweli mtupu, wala humjali mtu yeyote. Wala cheo cha mtu si kitu kwako, lakini wafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu. Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la? Tulipe au tusilipe?” Lakini Yesu alijua unafiki wao, akawaambia, “Mbona mnanijaribu? Nionesheni hiyo sarafu.” Wakamwonesha. Naye akawauliza, “Sura na chapa hii ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Basi, Yesu akawaambia, “Ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.” Wakashangazwa sana naye. Masadukayo ambao husema kwamba hakuna ufufuo walimwendea Yesu, wakamwuliza, “Mwalimu, Mose alituagiza hivi: ‘Mtu akifa na kuacha mke bila mtoto, ndugu yake lazima amchukue huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto.’ Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa, akafa bila kuacha mtoto. Ndugu wa pili akamwoa huyo mjane, naye pia akafa bila kuacha mtoto; na ndugu watatu hali kadhalika. Wote saba walikufa bila kuacha mtoto. Mwishowe yule mama mjane naye akafa. Basi, siku watu watakapofufuka, mama huyo atakuwa mke wa nani? Wote saba walikuwa wamemwoa.” Yesu akawaambia, “Nyinyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu. Maana wafu watakapofufuka hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika wa mbinguni. Lakini kuhusu kufufuliwa kwa wafu, je, hamjasoma kitabu cha Mose katika sehemu inayohusu kile kichaka kilichokuwa kinawaka moto? Mungu alimwambia Mose, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo.’ Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Nyinyi mmekosea sana.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Marko 12:13-27

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha