Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 10:32-45

Marko 10:32-45 BHN

Basi, walikuwa njiani kwenda juu Yerusalemu, na Yesu alikuwa anawatangulia. Wanafunzi wake walijawa na hofu, na watu waliofuata waliogopa. Yesu akawachukua tena kando wale kumi na wawili, akaanza kuwaambia yale yatakayompata: “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na waalimu wa sheria, nao watamhukumu auawe na kumkabidhi kwa watu wa mataifa. Nao watamdhihaki; watamtemea mate, watampiga mijeledi na kumuua. Lakini baada ya siku tatu atafufuka.” Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba.” Yesu akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” Wakamjibu, “Uturuhusu kuketi mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wako.” Yesu akawaambia, “Hamjui mnaomba nini! Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa, au kubatizwa kama nitakavyobatizwa?” Wakamjibu, “Tunaweza.” Yesu akawaambia, “Kikombe nitakachokunywa mtakinywa kweli, na mtabatizwa kama nitakavyobatizwa. Lakini ni nani atakayeketi kulia au kushoto kwangu si wajibu wangu kupanga bali nafasi hizo watapewa wale waliotayarishiwa.” Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, walianza kuchukizwa na Yakobo na Yohane. Hivyo, Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba wale wanaofikiriwa kuwa watawala wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao. Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkubwa kati yenu, sharti awe mtumishi wenu. Anayetaka kuwa wa kwanza, sharti awe mtumishi wa wote. Maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, ila kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.”