Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 2:1-12

Mathayo 2:1-12 BHN

Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu, mkoani Yudea, wakati Herode alipokuwa mfalme. Punde tu baada ya kuzaliwa kwake, wataalamu wa nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu, wakauliza, “Yuko wapi mtoto, Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona nyota yake ilipotokea mashariki, tukaja kumwabudu.” Mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, yeye pamoja na wakazi wote wa Yerusalemu. Basi, akawaita pamoja makuhani wakuu wote na waalimu wa sheria, akawauliza, “Kristo atazaliwa wapi?” Nao wakamjibu, “Mjini Bethlehemu, mkoani Yudea. Ndivyo nabii alivyoandika: ‘Ee Bethlehemu nchini Yudea, wewe si mdogo kamwe kati ya miji maarufu ya Yudea; maana kwako atatokea kiongozi atakayewaongoza watu wangu, Israeli.’” Hapo, Herode aliwaita faraghani hao wataalamu wa nyota, akawauliza wakati hasa ile nyota ilipowatokea. Kisha akawatuma Bethlehemu akisema, “Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto huyo. Mkisha mpata nileteeni habari ili nami niende kumwabudu.” Baada ya kumsikiliza mfalme, hao wataalamu wa nyota wakaenda. Kumbe ile nyota waliyokuwa wameiona upande wa mashariki iliwatangulia hata ikaenda kusimama juu ya mahali pale alipokuwa mtoto. Walipoiona hiyo nyota, walifurahi mno. Basi, wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi: Dhahabu, ubani na manemane. Mungu aliwaonya katika ndoto wasimrudie Herode; hivyo wakarudi makwao kwa njia nyingine.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha