Mathayo 12:1-21
Mathayo 12:1-21 BHN
Wakati huo, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano siku ya Sabato. Basi, wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakala punje zake. Mafarisayo walipoona hayo, wakamwambia Yesu, “Tazama, wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanya siku ya Sabato.” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu akala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Yeye wala hao wenzake hawakuruhusiwa kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani peke yao. Au je, hamjasoma katika kitabu cha sheria kwamba kila siku ya Sabato makuhani huivunja sheria hekaluni, lakini hawafikiriwi kuwa na hatia? Basi, nawaambieni kwamba hapa pana kikuu kuliko hekalu. Kama tu mngejua maana ya maneno haya: ‘Nataka huruma wala si tambiko,’ hamngewahukumu watu wasio na hatia. Maana Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.” Yesu alitoka hapo, akaenda katika sunagogi lao. Kulikuwa na mtu mmoja mwenye mkono uliopooza. Basi, watu wakamwuliza Yesu, “Je, ni halali kumponya mtu siku ya Sabato?” Walimwuliza hivyo wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akawaambia, “Tuseme mmoja wenu ana kondoo wake ambaye ametumbukia shimoni; je, hatamshika na kumtoa humo siku ya Sabato? Lakini, mtu ana thamani kuliko kondoo! Basi, ni halali kutenda mema siku ya Sabato.” Kisha akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha, nao ukawa mzima kabisa kama ule mwingine. Basi, Mafarisayo wakatoka nje, wakashauriana jinsi watakavyomwangamiza Yesu. Lakini Yesu alipojua jambo hilo, akatoka mahali pale. Watu wengi walimfuata, akawaponya wagonjwa wote, akawaamuru wasiwaambie watu habari zake, ili yale aliyosema Mungu kwa njia ya nabii Isaya yatimie: “Tazama mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote. Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale. Kwake yeye mataifa yatakuwa na matumaini.”