Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 12:1-21

Mathayo 12:1-21 NEN

Wakati huo Yesu alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala. Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa? Aliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani peke yao. Au hamjasoma katika Sheria kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia? Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa. Kama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia, kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.” Yesu akaondoka mahali hapo, akaingia ndani ya sinagogi lao, na huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, wakamuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?” Yesu akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa? Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.” Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine. Lakini Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri baya juu ya Yesu jinsi watakavyoweza kumuua. Lakini Yesu alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi wakamfuata, naye akawaponya wagonjwa wao wote, akiwakataza wasiseme yeye ni nani. Hii ilikuwa ili litimie lile neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kusema: “Tazama mtumishi wangu niliyemchagua, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Nitaweka Roho wangu juu yake, naye atatangaza haki kwa mataifa. Hatagombana wala hatapiga kelele, wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, na utambi unaofuka moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya haki ishinde. Katika Jina lake mataifa wataweka tumaini lao.”