Mathayo 1:18-24
Mathayo 1:18-24 BHN
Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri. Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, “Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye ndiye atakayewaokoa watu wake katika dhambi zao.” Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii: “Bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto wa kiume, nao watampa jina Emanueli” (maana yake, “Mungu yuko nasi”). Hivyo, Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia, akamchukua mke wake nyumbani.