Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 1:1-23

Mathayo 1:1-23 BHN

Yesu Kristo alikuwa wa ukoo wa Daudi, wa ukoo wa Abrahamu. Hii ndiyo orodha ya ukoo wake: Abrahamu alimzaa Isaka, Isaka alimzaa Yakobo, Yakobo alimzaa Yuda na ndugu zake, Yuda alimzaa Peresi na Zera (mama yao alikuwa Tamari), Peresi alimzaa Hesroni, Hesroni alimzaa Rami, Rami alimzaa Aminadabu, Aminadabu alimzaa Nashoni, Nashoni alimzaa Salmoni, Salmoni alimzaa Boazi (mama yake Boazi alikuwa Rahabu) Boazi na Ruthu walikuwa wazazi wa Obedi, Obedi alimzaa Yese, naye Yese alimzaa Mfalme Daudi. Daudi alimzaa Solomoni (mama yake Solomoni alikuwa Bath-Sheba mke wa Uria). Solomoni alimzaa Rehoboamu, Rehoboamu alimzaa Abiya, Abiya alimzaa Asa, Asa alimzaa Yehoshafati, Yehoshafati alimzaa Yoramu, Yoramu alimzaa Uzia, Uzia alimzaa Yothamu, Yothamu alimzaa Ahazi, Ahazi alimzaa Hezekia, Hezekia alimzaa Manase, Manase alimzaa Amoni, Amoni alimzaa Yosia, Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake. Huo ulikuwa wakati Wayahudi walipopelekwa uhamishoni Babuloni. Baada ya Wayahudi kupelekwa uhamishoni Babuloni, Yekonia alimzaa Shealtieli, Shealtieli alimzaa Zerubabeli, Zerubabeli alimzaa Abiudi, Abiudi alimzaa Eliakimu, Eliakimu alimzaa Azori, Azori alimzaa Zadoki, Zadoki alimzaa Akimu, Akimu alimzaa Eliudi, Eliudi alimzaa Eleazari, Eleazari alimzaa Mathani, Mathani alimzaa Yakobo, Yakobo alimzaa Yosefu, mumewe Maria mama yake Yesu aitwaye Kristo. Basi, kulikuwa na vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi mpaka Wayahudi walipochukuliwa mateka Babuloni, na vizazi kumi na vinne tangu kuchukuliwa mateka mpaka wakati wa Kristo. Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri. Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, “Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye ndiye atakayewaokoa watu wake katika dhambi zao.” Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii: “Bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto wa kiume, nao watampa jina Emanueli” (maana yake, “Mungu yuko nasi”).