Luka 8:22-56
Luka 8:22-56 BHN
Siku moja, Yesu alipanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Tuvuke ziwa twende mpaka ngambo.” Basi, wakaanza safari. Walipokuwa wanasafiri kwa mashua, Yesu alishikwa na usingizi, akalala. Dhoruba kali ikaanza kuvuma, maji yakaanza kuingia ndani ya mashua, wakawa katika hatari. Wale wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwamsha wakisema, “Bwana, Bwana! Tunaangamia!” Yesu akaamka, akaukemea upepo na mawimbi ya maji, navyo vikatulia, kukawa shwari. Kisha akawaambia, “Iko wapi imani yenu?” Lakini wao walishangaa na kuogopa huku wakiambiana, “Huyu ni nani basi, hata anaamuru dhoruba na mawimbi, navyo vinamtii?” Wakaendelea na safari, wakafika pwani ya nchi ya Wagerase inayokabiliana na Galilaya, ngambo ya ziwa. Alipokuwa anashuka pwani, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo alimjia kutoka mjini. Kwa muda mrefu mtu huyo hakuwa anavaa nguo, wala hakuwa anaishi nyumbani bali makaburini. Alipomwona Yesu, alijitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kubwa, “We, Yesu Mwana wa Mungu Mkuu, una shauri gani nami? Ninakusihi usinitese!” Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia huyo pepo mchafu amtoke mtu huyo. Pepo huyo mchafu alikuwa anamvamia mtu huyo mara nyingi, na ingawa watu walimweka ndani na kumfunga kwa minyororo na pingu, lakini kila mara alivivunja vifungo hivyo, akakimbizwa na pepo huyo mchafu hadi jangwani. Basi, Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?” Yeye akajibu, “Jina langu ni ‘Jeshi’” – kwa sababu pepo wengi walikuwa wamempagaa. Hao pepo wakamsihi asiwapeleke kwenye shimo kuu. Mahali hapo kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha mlimani. Basi, hao pepo wakamsihi awaruhusu wawaingie. Naye Yesu akawapa ruhusa. Kwa hiyo pepo hao wakamtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nao wakaporomoka kwenye ule mteremko mkali, wakatumbukia ziwani, wakafa maji. Wale wachungaji walipoona yote yaliyotokea walikimbia, wakaenda kuwapa watu habari mjini na mashambani. Watu wakaja kuona yaliyotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mtu aliyetokwa na pepo ameketi karibu na Yesu, amevaa nguo, ana akili zake, wakaogopa. Wale watu walioshuhudia tukio hilo waliwaeleza hao jinsi yule mtu alivyoponywa. Wakazi wa nchi ya Gerase walishikwa na hofu kubwa. Kwa hiyo wakamwomba Yesu aondoke, aende zake. Hivyo Yesu alipanda tena mashua, akaondoka. Yule mtu aliyetokwa na wale pepo akamsihi aende pamoja naye. Lakini Yesu hakumruhusu, bali akamwambia, “Rudi nyumbani ukaeleze yote Mungu aliyokutendea.” Basi, yule mtu akaenda akitangaza kila mahali katika mji ule mambo yote Yesu aliyomtendea. Yesu aliporudi upande mwingine wa ziwa, kundi la watu lilimkaribisha, kwa maana wote walikuwa wanamngojea. Hapo akaja mtu mmoja aitwaye Yairo, ofisa wa sunagogi. Alijitupa miguuni pa Yesu, akamwomba aende nyumbani kwake, kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa. Yesu alipokuwa akienda, watu wakawa wanamsonga kila upande. Basi, kulikuwa na mwanamke mmoja kati ya lile kundi la watu, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili; ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote kwa waganga, hakuna aliyefaulu kumponya. Huyo mwanamke alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake. Papo hapo akaponywa ugonjwa wake wa kutokwa damu. Yesu akasema, “Ni nani aliyenigusa?” Wote wakasema kwamba hapakuwa na mtu aliyemgusa. Naye Petro akasema, “Bwana, umati wa watu umekuzunguka na kukusonga!” Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, maana nimehisi nguvu imenitoka.” Yule mwanamke alipoona kwamba hawezi kujificha, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa mbele ya Yesu. Hapo akaeleza mbele ya wote kisa cha kumgusa Yesu na jinsi alivyoponywa mara moja. Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda na amani.” Alipokuwa bado akiongea, Yairo akaletewa habari kutoka nyumbani: “Binti yako amekwisha kufa, ya nini kumsumbua Mwalimu zaidi?” Yesu aliposikia hayo akamwambia Yairo, “Usiogope; amini tu, naye atapona.” Alipofika nyumbani hakumruhusu mtu kuingia ndani pamoja naye, isipokuwa Petro, Yohane, Yakobo na wazazi wa huyo msichana. Watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili yake. Lakini Yesu akawaambia, “Msilie, kwa maana mtoto hajafa, amelala tu!” Nao wakamcheka kwa sababu walijua kwamba alikuwa amekufa. Lakini Yesu akamshika mkono akasema, “Mtoto, amka!” Roho yake ikamrudia, akaamka mara. Yesu akaamuru wampe chakula. Wazazi wake walishangaa, lakini Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote hayo yaliyotendeka.