Lk 8:22-56
Lk 8:22-56 SUV
Ikawa siku zile mojawapo alipanda chomboni yeye na wanafunzi wake, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo ya ziwa. Wakatweka matanga. Nao walipokuwa wakienda, alilala usingizi. Ikashuka tufani juu ya ziwa, chombo kikaanza kujaa maji, wakawa katika hatari. Wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana mkubwa, Bwana mkubwa, tunaangamia. Akaamka, akaukemea upepo na msukosuko wa maji, vikakoma; kukawa shwari. Akawaambia, Imani yenu iko wapi? Wakaogopa, wakamaka, wakisema wao kwa wao, Ni nani huyu basi hata anaamuru upepo na maji, navyo vyamtii? Wakafika pwani ya nchi ya Wagerasi, inayoelekea Galilaya. Naye aliposhuka pwani, alikutana na mtu mmoja wa mji ule, mwenye pepo, hakuvaa nguo siku nyingi, wala hakukaa nyumbani, ila makaburini. Alipomwona Yesu alipiga kelele, akaanguka mbele yake, akasema kwa sauti kuu, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakusihi usinitese. Kwa kuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke mtu yule. Maana amepagawa naye mara nyingi, hata alilindwa kifungoni na kufungwa minyororo na pingu; akavikata vile vifungo, akakimbizwa jangwani kwa nguvu za yule pepo. Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia. Wakamsihi asiwaamuru watoke kwenda shimoni. Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa. Pepo wakamtoka mtu yule wakawaingia nguruwe, nalo kundi lilitelemka gengeni kwa kasi, wakaingia ziwani, wakafa maji. Wachungaji walipoona lililotokea walikimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka kwenda kuliona lililotokea, wakamwendea Yesu, wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi miguuni pa Yesu, amevaa nguo, ana akili zake; wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza jinsi alivyoponywa yule aliyepagawa na pepo. Na jamii ya watu wa nchi ya Wagerasi iliyo kando kando walimwomba aondoke kwao, kwa kuwa walishikwa na hofu nyingi; basi akapanda chomboni, akarudi. Na mtu yule aliyetokwa na pepo alimwomba ruhusa afuatane naye; lakini yeye alimwaga akisema, Rudi nyumbani kwako, ukahubiri yalivyo makuu Mungu aliyokutendea. Akaenda zake, akihubiri katika mji wote, yalivyo makuu mambo aliyotendewa na Yesu. Basi Yesu aliporudi mkutano ulimkaribisha kwa furaha, maana walikuwa wakimngojea wote. Na tazama, mtu mmoja akaja, jina lake Yairo, naye ni mtu mkuu wa sinagogi, akaanguka miguuni pa Yesu, akamsihi aingie nyumbani kwake; kwa kuwa binti yake yu katika kufa, ambaye ni mwana pekee, umri wake amepata miaka kumi na miwili. Na alipokuwa akienda makutano walimsonga. Na mwanamke mmoja, ambaye ametokwa na damu muda wa miaka kumi na miwili, [aliyekuwa amegharimiwa mali zake zote kwa kuwapa waganga] asipate kuponywa na mtu ye yote, alikwenda nyuma yake, akaugusa upindo wa vazi lake; na mara hiyo kutoka damu kwake kulikoma. Yesu akasema, Ni nani aliyenigusa? Basi, watu wote walipokana, Petro alimwambia, Bwana mkubwa, makutano haya wanakuzunguka na kukusonga. Yesu akasema, Mtu alinigusa, maana naona ya kuwa nguvu zimenitoka. Yule mwanamke, alipoona ya kwamba hawezi kusitirika akaja akitetemeka, akaanguka mbele yake, akamweleza mbele ya watu wote sababu yake ya kumgusa, na jinsi alivyoponywa mara. Akamwambia Binti, imani yako imekuponya; enenda zako na amani. Alipokuwa akinena hayo, alikuja mtu kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akamwambia, Binti yako amekwisha kufa; usimsumbue mwalimu. Lakini Yesu aliposikia hayo, alimjibu, Usiwe na hofu, amini tu, naye ataponywa. Alipofika nyumbani hakuacha mtu kuingia pamoja naye ila Petro, na Yohana, na Yakobo, na babaye yule mtoto na mamaye. Na watu wote walikuwa wakilia na kumwombolezea; akasema, Msilie, hakufa huyu, bali amelala usingizi tu. Wakamcheka sana, maana walijua ya kuwa amekwisha kufa. Akamshika mkono, akapaza sauti, akisema Kijana, inuka. Roho yake ikamrejea, naye mara hiyo akasimama. Akaamuru apewe chakula. Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini akawakataza wasimwambie mtu lililotukia.