Luka 7:11-23
Luka 7:11-23 BHN
Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja uitwao Naini, na wafuasi wake na kundi kubwa la watu waliandamana naye. Basi, alipokuwa anakaribia lango la mji, walitokea watu wamebeba maiti ya mwanamume mmoja, mtoto wa pekee wa mama mjane. Watu wengi wa mji ule walikuwa pamoja na huyo mama. Bwana alipomwona mama huyo akamwonea huruma, akamwambia, “Usilie.” Kisha, akaenda akaligusa lile jeneza, na wale waliokuwa wamelichukua wakasimama. Halafu akasema, “Kijana! Nakuamuru, amka!” Yule aliyekufa akaketi, akaanza kuongea. Na Yesu akamkabidhi kwa mama yake. Watu wote walishikwa na hofu, wakawa wanamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea kati yetu. Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.” Habari hizo zikaenea kote katika Yudea na katika nchi za jirani. Wanafunzi wa Yohane walimhabarisha Yohane juu ya mambo hayo yote. Naye Yohane, baada ya kuwaita wawili kati ya wanafunzi wake, aliwatuma kwa Bwana wamwulize: “Wewe ndiye yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Wale wanafunzi walipomfikia Yesu wakamwambia, “Yohane Mbatizaji ametutuma kwako tukuulize: ‘Wewe ndiye yule anayekuja, au tumngoje mwingine?’” Wakati huohuo, Yesu alikuwa anawaponya watu wengi waliokuwa wanateseka kwa magonjwa na waliopagawa na pepo wabaya na kuwawezesha vipofu wengi kuona. Basi, Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane yale mliyojionea na kuyasikia: Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami!”