Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 7:11-23

Luka 7:11-23 NEN

Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja ulioitwa Naini. Nao wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu walikwenda pamoja naye. Alipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule ulikuwa pamoja na huyo mwanamke. Bwana Yesu alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.” Kisha akasogea mbele akaligusa lile jeneza na wale waliokuwa wamelibeba wakasimama kimya. Akasema, “Kijana, nakuambia inuka.” Yule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Yesu akamkabidhi kwa mama yake. Watu wote wakajawa na hofu ya Mungu, nao wakamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea miongoni mwetu, Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.” Habari hizi za mambo aliyoyafanya Yesu zikaenea Uyahudi wote na sehemu zote za jirani. Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji wakamweleza Yohana mambo haya yote. Hivyo Yohana akawaita wanafunzi wake wawili na kuwatuma kwa Bwana ili kumuuliza, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?” Wale watu walipofika kwa Yesu wakamwambia, “Yohana Mbatizaji ametutuma tukuulize, ‘Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?’ ” Wakati huo huo, Yesu aliwaponya wengi waliokuwa na magonjwa, maradhi na pepo wachafu, na pia akawafungua vipofu wengi macho wakapata kuona. Hivyo akawajibu wale wajumbe, “Rudini mkamwambie Yohana yote mnayoyaona na kuyasikia: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema. Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Luka 7:11-23