Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 20:1-26

Luka 20:1-26 BHN

Siku moja, Yesu alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni na kuwahubiria juu ya Habari Njema, makuhani wakuu na waalimu wa sheria pamoja na wazee walifika, wakasema, “Tuambie! Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani?” Yesu akawaambia, “Na mimi nitawaulizeni swali: Mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa Mungu au kwa watu?” Lakini wao wakajadiliana hivi: “Tukisema yalitoka kwa Mungu, yeye atatuuliza: ‘Mbona hamkumsadiki?’ Na tukisema yalitoka kwa binadamu, watu wote hapa watatupiga mawe, maana wote wanaamini kwamba Yohane alikuwa nabii.” Basi, wakamwambia, “Hatujui mamlaka hayo yalitoka wapi.” Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.” Yesu akaendelea kuwaambia watu mfano huu: “Mtu mmoja alilima shamba la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima; kisha akasafiri hadi nchi ya mbali, akakaa huko kwa muda mrefu. Wakati wa mavuno, mtu huyo alimtuma mtumishi wake kwa wale wakulima, akachukue sehemu ya matunda ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima wakampiga mtumishi huyo, wakamrudisha mikono mitupu. Yule bwana akamtuma tena mtumishi mwingine; lakini wao wakampiga huyo vilevile na kumtendea vibaya, wakamrudisha mikono mitupu. Akamtuma tena wa tatu; huyu naye, baada ya kumwumiza, wakamfukuza. Yule mwenye shamba akafikiri: ‘Nitafanya nini? Nitamtuma mwanangu mpenzi; labda watamjali yeye.’ Wale wakulima walipomwona tu, wakasemezana: ‘Huyu ndiye mrithi. Basi, tumuue ili urithi wake uwe wetu.’ Basi, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamuua.” Yesu akauliza, “Yule mwenye shamba atawafanya nini hao wakulima? Atakuja kuwaangamiza wakulima hao, na kuwapa wakulima wengine hilo shamba la mizabibu.” Watu waliposikia maneno hayo, walisema: “Hasha! Yasitukie hata kidogo!” Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Maandiko haya Matakatifu yana maana gani, basi? ‘Jiwe walilokataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi!’ Mtu yeyote akianguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda.” Waalimu wa sheria na makuhani wakuu walifahamu kwamba mfano huo ulikuwa unawahusu, na hivyo walitaka kumkamata palepale, ila tu waliogopa watu. Basi, wakawa wanatafuta wakati wa kufaa. Wakawahonga watu fulani wajisingizie kuwa wema, wakawatuma wamnase Yesu kwa maswali, na hivyo waweze kumtia nguvuni na kumpeleka kwa wakuu wa serikali. Hao wapelelezi wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba unasema na kufundisha mambo ya kweli; tunajua kwamba wewe huna ubaguzi; wewe wafundisha ukweli juu ya njia ya Mungu. Basi, tuambie kama ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari!” Yesu alitambua mtego wao, akawaambia, “Nionesheni sarafu. Je, sura na chapa ni vya nani?” Nao wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.” Hawakufaulu kumnasa kwa neno lolote pale mbele ya watu na hivyo wakakaa kimya wakilistaajabia jibu lake.