Luka 12:22-28
Luka 12:22-28 BHN
Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi. Chukueni kwa mfano, kunguru: Hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Nyinyi mna thamani zaidi kuliko ndege! Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuongeza kidogo urefu wa maisha yake? Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine? Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo. Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba!