Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Walawi UTANGULIZI

UTANGULIZI
Kitabu hiki cha tatu katika vitabu vitano vya Mose (au “Pentateuko”) kimepewa jina “Walawi” na tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX).
Katika aya ya kwanza ya sura ya kwanza ya kitabu hiki, tunaambiwa kwamba Mungu anamwita Mose aende kuongea naye katika hema la mkutano. Kitabu chote kinahusu hasa idadi kubwa ya sheria au kanuni ambazo Mungu aliwapa Waisraeli na kuwaahidi kwamba wale watakaotekeleza kanuni na maongozi hayo wataishi kwazo (taz 18:5, aya ambayo imekaririwa katika Rom 10:5.)
Kwa jumla, jambo la msingi katika kitabu hiki ni juu ya utakatifu wake Mungu mwenyewe na kwa sababu ya utakatifu huo wa Mungu, nao watu wake wanapaswa kuwa watakatifu: “Ni lazima muwe watakatifu kwani mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ni mtakatifu” (19:2). Kwa hiyo maagizo na kanuni zinazotajwa katika kitabu hiki zilikuwa na shabaha ya kusimika duniani taifa ambalo limewekwa wakfu kwa Mungu mwenyewe, watu ambao walitakiwa kumwabudu na kushika au kudumisha uhusiano wao naye ambaye ndiye aliye Mtakatifu wa Israeli. Kwamba yeyote anayemtolea sadaka yambidi kufanya hivyo kulingana na masharti au sheria (sura 17), kwamba makuhani ni lazima waheshimiwe na wao wajistahi inavyotakiwa (sura 8-10) na kwamba kila mmoja wa hiyo jumuiya ya Waisraeli lazima ajiepushe kadiri iwezekanavyo na kitu chochote kilicho najisi (sura 11-16), waepukane na maisha mapotovu na ibada zisizokubalika (sura 17-27). Hatimaye, Waisraeli wanapewa amri ambayo Yesu mwenyewe alikariri: “Umpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe” (19:18; tazama Mat 22:29).
Sheria hizo ambazo kwa msomaji wa siku hizi zaonekana ngeni, zinawakumbusha watu kwamba uhusiano mwema kati ya Mungu na watu wake ni jambo muhimu na la kuzingatia.

Iliyochaguliwa sasa

Walawi UTANGULIZI: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia