Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoeli 2:18-27

Yoeli 2:18-27 BHN

Ndipo Mwenyezi-Mungu akaipenda nchi yake akawahurumia watu wake. Alisikiliza, akajibu sala zao; akasema, “Sasa nitawapeni tena nafaka, sitawafanya mdharauliwe tena na mataifa. Nitawaondoa hao adui watokao kaskazini, nitawafukuza mpaka jangwani; askari wa mbele nitawatupa katika Bahari ya Chumvi na wale wa nyuma katika Bahari ya Mediteranea. Watatoa uvundo na harufu mbaya, hao ambao wamefanya maovu makubwa. “Usiogope, ewe nchi, bali furahi na kushangilia, maana Mwenyezi-Mungu ametenda makuu. Msiogope, enyi wanyama. malisho ya nyikani yamekuwa mazuri, miti inazaa matunda yake, mizabibu na mitini zinazaa kwa wingi. “Furahini, enyi watu wa Siyoni, shangilieni kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, maana amewapeni mvua za masika, amewapeni mvua ya kutosha: Mvua za masika na mvua za vuli kama hapo awali. Mahali pa kupuria patajaa nafaka, mashinikizo yatafurika divai na mafuta. Nitawarudishia miaka ile iliyoliwa na nzige, kila kitu kilicholiwa na tunutu, parare na matumatu, hilo jeshi kubwa nililowaletea! Mtapata chakula kingi na kutosheka; mtalisifu jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu. Watu wangu, kamwe hawatadharauliwa tena. Mtatambua kwamba mimi nimo miongoni mwenu, enyi Waisraeli; kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, ndimi Mungu wenu wala hakuna mwingine. Watu wangu, kamwe hawatadharauliwa tena.

Soma Yoeli 2

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yoeli 2:18-27