Yobu 38:4-11
Yobu 38:4-11 BHN
“Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya dunia? Niambie, kama una maarifa. Ni nani aliyeweka vipimo vyake, wajua bila shaka! Au nani aliyelaza kamba juu yake kuipima? Je, nguzo za dunia zimesimikwa juu ya nini, au nani aliyeliweka jiwe lake la msingi, nyota za asubuhi zilipokuwa zikiimba pamoja, na wana wa Mungu wakapaza sauti za shangwe? Ni nani aliyeyafunga mafuriko ya bahari wakati yalipozuka na kuvuma kutoka vilindini? Mimi ndiye niliyeifunika bahari kwa mawingu na kuiviringishia giza nene. Niliiwekea bahari mipaka, nikaizuia kwa makomeo na milango, nikaiambia: ‘Mwisho wako ni hapa, si zaidi! Mawimbi yako ya nguvu yatakomea hapa!’