Yobu 2
2
Jaribio la pili
1Ikatokea tena siku nyingine, malaika wa Mungu walikwenda kukutana mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye Shetani akajitokeza pia pamoja nao.
2Mwenyezi-Mungu akamwuliza Shetani, “Umetoka wapi wewe?” Naye Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Nimetoka kutembeatembea na kuzungukazunguka duniani.” 3Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia mtumishi wangu Yobu? Duniani hakuna mwingine aliye kama yeye. Yeye ni mtu mnyofu, mcha Mungu na mwenye kujiepusha na uovu. Yeye yuko imara katika unyofu wake, ingawa wewe umenichochea nimwangamize bure.”
4Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Ngozi kwa ngozi!#2:4 Ngozi kwa ngozi! Maana yake si dhahiri. Labda methali yenye maana: Yaliyofanyika mpaka sasa hayagusi hali ya ndani. Mtu hutoa kila kitu alicho nacho ili aokoe uhai wake. 5Lakini sasa hebu nyosha mkono wako umguse mwili wake; nakuambia atakutukana waziwazi.” 6Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Haya! Waweza kumfanya utakavyo, walakini usimuue.”
7Hapo Shetani akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamtesa Yobu kwa madonda mabaya tangu wayo wa mguu wake mpaka utosini mwake. 8Yobu akatwaa kigae, akajikuna nacho na kuketi kwenye majivu. 9Mkewe akamwambia, “Bado tu ungali ukishikilia unyofu wako? Mtukane Mungu, ufe.”
10Yobu akamjibu mkewe, “Wewe unaongea kama wanawake wapumbavu. Tukipokea mema kutoka kwa Mungu, kwa nini tukatae kupokea pia mabaya kutoka kwake?” Katika mambo hayo yote, Yobu hakutamka neno lolote la kumkosea Mungu.
Marafiki watatu wa Yobu wawasili
11Marafiki watatu wa Yobu: Elifazi kutoka Temani, Bildadi kutoka Shua na Sofari kutoka Naamathi, walisikia juu ya maafa yote yaliyompata Yobu. Basi, wakaamua kwa pamoja waende kumpa pole na kumfariji. 12Walipomwona kwa mbali hawakumtambua. Basi, wakaanza kupaza sauti na kulia; waliyararua mavazi yao, wakarusha mavumbi angani na juu ya vichwa vyao. 13Kisha wakaketi udongoni pamoja na Yobu kwa siku saba, mchana na usiku, bila kumwambia neno lolote kwani waliyaona mateso yake kuwa makubwa mno.
Iliyochaguliwa sasa
Yobu 2: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.