Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 9:1-25

Yohane 9:1-25 BHN

Yesu alipokuwa akipita alimwona mtu mmoja, kipofu tangu kuzaliwa. Basi, wanafunzi wakamwuliza, “Mwalimu! Ni nani aliyetenda dhambi: Mtu huyu, ama wazazi wake, hata akazaliwa kipofu?” Yesu akajibu, “Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye, wala dhambi za wazazi wake; ila alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake. Kukiwa bado mchana yatupasa kuendelea kufanya kazi za yule aliyenituma; maana usiku unakuja ambapo mtu hawezi kufanya kazi. Wakati ningali ulimwenguni, mimi ni mwanga wa ulimwengu.” Baada ya kusema hayo, akatema mate chini, akafanyiza tope, akampaka yule kipofu machoni, akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (Maana ya jina hili ni “aliyetumwa”). Hapo, huyo kipofu akaenda, akanawa, kisha akarudi akiwa anaona. Basi, jirani zake na wale waliokuwa wanajua kwamba hapo awali alikuwa maskini mwombaji, wakasema, “Je, huyu siye yule maskini aliyekuwa akiketi na kuomba?” Baadhi yao wakasema, “Ndiye.” Wengine wakasema, “La! Ila anafanana naye.” Lakini huyo aliyekuwa kipofu akasema, “Ni mimi!” Basi, wakamwuliza, “Sasa, macho yako yalipataje kufumbuliwa?” Naye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni na kuniambia: ‘Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.’ Hapo, mimi nikaenda, nikanawa, nikapata kuona.” Wakamwuliza, “Yeye yuko wapi?” Naye akawajibu, “Mimi sijui!” Kisha wakampeleka huyo mtu aliyekuwa kipofu kwa Mafarisayo. Siku hiyo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho mtu huyo, ilikuwa siku ya Sabato. Basi, Mafarisayo wakamwuliza mtu huyo, “Umepataje kuona?” Naye akawaambia, “Alinipaka tope machoni, nami nikanawa na sasa naona.” Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Mtu huyu hakutoka kwa Mungu, maana hashiki sheria ya Sabato.” Lakini wengine wakasema, “Mtu mwenye dhambi awezaje kufanya ishara za namna hii?” Kukawa na mafarakano kati yao. Wakamwuliza tena huyo mtu aliyekuwa kipofu, “Maadamu yeye amekufungua macho, wasemaje juu yake?” Naye akawaambia, “Yeye ni nabii!” Viongozi wa Wayahudi hawakusadiki kwamba mtu huyo alikuwa kipofu hapo awali na sasa anaona, mpaka walipowaita wazazi wake. Basi, wakawauliza hao wazazi, “Je, huyu ndiye mtoto wenu ambaye nyinyi mwasema alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona?” Wazazi wake wakajibu, “Tunajua kwamba huyu ni mtoto wetu, na kwamba alizaliwa kipofu. Lakini amepataje kuona, hatujui; na wala hatumjui yule aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima, anaweza kujitetea mwenyewe.” Wazazi wake walisema hivyo kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi kwani viongozi hao walikuwa wamepatana ya kwamba mtu yeyote atakayekiri kwamba Yesu ni Kristo atafukuzwa nje ya sunagogi. Ndiyo maana wazazi wake walisema: “Yeye ni mtu mzima, mwulizeni.” Basi, wakamwita tena huyo aliyekuwa kipofu, wakamwambia, “Sema ukweli mbele ya Mungu! Sisi tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi.” Yeye akajibu, “Kama ni mwenye dhambi mimi sijui. Lakini kitu kimoja najua: Nilikuwa kipofu, na sasa naona.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yohane 9:1-25