Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 9:1-25

Yohana 9:1-25 SRUV

Na alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake. Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi. Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu. Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope machoni, akamwambia, Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi akiwa anaona. Basi jirani zake, na wale waliomwona zamani kuwa ni mwombaji, wakasema, Je! Huyu siye yule aliyekuwa akiketi na kuomba? Wengine wakasema, Ndiye. Wengine wakasema, La, lakini amefanana naye. Yeye mwenyewe alisema, Mimi ndiye. Basi wakamwambia, Macho yako yalifumbuliwaje? Yeye akajibu, Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka macho akaniambia, Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona. Wakamwambia, Yuko wapi huyo? Akasema, Mimi sijui. Basi wakampeleka kwa Mafarisayo yule aliyekuwa kipofu zamani. Nayo ilikuwa sabato, hapo Yesu alipofanya zile tope na kumfumbua macho. Basi Mafarisayo nao wakamwuliza tena jinsi gani alivyopata kuona. Akawaambia, Alinitia tope juu ya macho, nami nikanawa, na sasa naona. Basi baadhi ya Mafarisayo wakasema, Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki sabato. Wengine wakasema, Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya ishara kama hizo? Kukawa na utengano kati yao. Basi wakamwambia yule kipofu mara ya pili, Wewe wasemaje kuhusu habari zake kwa vile alivyokufumbua macho? Akasema, Ni nabii. Basi Wayahudi hawakuamini habari zake, ya kuwa alikuwa kipofu, kisha akapata kuona; hadi walipowaita wazazi wake yule aliyepata kuona. Wakawauliza wakisema, Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi, kuona sasa? Wazazi wake wakawajibu, wakasema, Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu; lakini jinsi aonavyo sasa hatujui; wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima; atajisemea mwenyewe. Wazazi wake waliyasema hayo kwa sababu waliwaogopa Wayahudi; kwa maana Wayahudi walikuwa wamekwisha kukubaliana kwamba mtu akimkiri kuwa ni Kristo, atatengwa na sinagogi. Ndiyo sababu wale wazazi wake walisema, Ni mtu mzima, mwulizeni yeye. Basi mara ya pili wakamwita yule mtu aliyekuwa kipofu, wakamwambia, Mpe Mungu utukufu. Sisi tunajua ya kuwa mtu huyo ni mwenye dhambi. Basi yule mtu akajibu, Kwamba yeye ni mwenye dhambi sijui. Najua neno moja, kuwa mimi nilikuwa kipofu na sasa naona.

Soma Yohana 9

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yohana 9:1-25