Yohane 7:1-31
Yohane 7:1-31 BHN
Baada ya hayo, Yesu alikuwa akitembea huko Galilaya. Hakutaka kutembea mkoani Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi walikuwa wanataka kumuua. Sikukuu ya Wayahudi ya vibanda ilikuwa imekaribia. Basi, ndugu zake wakamwambia, “Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi wako wazione kazi unazozifanya. Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa watu. Maadamu unafanya mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu.” (Hata ndugu zake hawakumwamini). Basi, Yesu akawaambia, “Wakati wangu ufaao haujafika bado. Lakini kwenu nyinyi kila wakati unafaa. Ulimwengu hauwezi kuwachukia nyinyi, lakini mimi wanichukia kwa sababu mimi nashuhudia juu yake kwamba matendo yake ni maovu. Nyinyi nendeni kwenye sikukuu hiyo. Mimi siendi kwenye sikukuu hiyo, maana saa yangu ifaayo haijafika.” Alisema hayo kisha akabaki huko Galilaya. Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri. Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; wakauliza, “Yuko wapi?” Kulikuwa na minongono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walisema, “La! Anawapotosha watu.” Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi. Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda hekaluni, akaanza kufundisha. Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema, “Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?” Hapo Yesu akawajibu, “Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma. Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe. Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote. Je, Mose hakuwapeni sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika sheria. Kwa nini mnataka kuniua?” Hapo watu wakamjibu, “Una pepo wewe! Nani anataka kukuua?” Yesu akawajibu, “Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia. Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa nyinyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato. Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi sheria isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya Sabato? Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki.” Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, “Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu? Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo? Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!” Basi, Yesu alipokuwa anafundisha hekaluni alipaza sauti na kusema, “Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui. Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.” Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, “Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?”