Yohane 6:15-21
Yohane 6:15-21 BHN
Yesu akajua kwamba watu walitaka kumchukua wamfanye mfalme, akaondoka tena, akaenda mlimani peke yake. Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani, wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu. Giza lilikuwa limeingia, na Yesu alikuwa hajawafikia bado. Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana. Yesu akawaambia, “Ni mimi, msiogope!” Basi wakataka kumchukua Yesu katika mashua; na mara mashua ikawasili nchi kavu walikokuwa wanakwenda.