Yohane 6:1-13
Yohane 6:1-13 BHN
Baada ya hayo, Yesu alivuka ziwa Galilaya (au ziwa Tiberia). Umati mkubwa wa watu ulimfuata kwa sababu watu hao walikuwa wameona ishara alizokuwa akifanya kwa kuwaponya wagonjwa. Yesu alipanda mlimani, akaketi pamoja na wanafunzi wake. Sikukuu ya Wayahudi iitwayo Pasaka ilikuwa imekaribia. Basi, Yesu alipotazama na kuona umati wa watu ukija kwake, alimwambia Filipo, “Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?” (Alisema hivyo kwa kumjaribu Filipo, kwani alijua mwenyewe atakalofanya.) Filipo akamjibu, “Mikate ya fedha dinari 200 haiwatoshi watu hawa hata kama kila mmoja atapata kipande kidogo tu!” Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, “Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?” Yesu akasema, “Waketisheni watu.” Palikuwa na nyasi tele mahali hapo. Basi, watu wakaketi, jumla yapata wanaume 5,000. Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri alivyotaka. Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee.” Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili.