Yohane 20:10-18
Yohane 20:10-18 BHN
Basi, hao wanafunzi wakarudi nyumbani. Maria alikuwa amesimama nje ya kaburi, akilia. Huku akiwa bado analia, aliinama na kuchungulia kaburini, akawaona malaika wawili waliovaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja kichwani na wa pili miguuni. Hao malaika wakamwuliza, “Mama, kwa nini unalia?” Naye akawaambia, “Wamemwondoa Bwana wangu, na wala sijui walikomweka!” Baada ya kusema hayo, aligeuka nyuma, akamwona Yesu amesimama hapo, lakini asitambue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwuliza, “Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?” Maria, akidhani kwamba huyo ni mtunza bustani, akamwambia, “Mheshimiwa, kama ni wewe umemwondoa, niambie ulikomweka, nami nitamchukua.” Yesu akamwambia, “Maria!” Naye Maria akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, “Raboni” (yaani “Mwalimu”). Yesu akamwambia, “Usinishike; sijaenda bado juu kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu uwaambie: Naenda juu kwa Baba yangu na Baba yenu, Mungu wangu na Mungu wenu.” Hivyo Maria Magdalene akaenda akawapasha habari wale wanafunzi kuwa amemwona Bwana, na kwamba alikuwa amemwambia hivyo.