Yohane 12:1-19
Yohane 12:1-19 BHN
Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alifika Bethania alikoishi Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua kutoka wafu. Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa anawatumikia. Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu. Basi, Maria alichukua nusu lita ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote ikajaa harufu ya marashi. Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema, “Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari 300, wakapewa maskini?” Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina. Lakini Yesu akasema, “Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu. Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote.” Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania. Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka kwa wafu. Makuhani wakuu waliamua pia kumwua Lazaro, maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini Yesu. Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu. Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaza sauti wakisema: “Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana. Abarikiwe mfalme wa Israeli.” Yesu akampata mwanapunda mmoja, akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko: “Usiogope mji wa Siyoni! Tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwanapunda!” Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo. Kundi la watu wale waliokuwa pamoja na Yesu wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka kwa wafu, walimshuhudia. Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo. Basi, Mafarisayo wakaambiana, “Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata.”