Yohana 12:1-19
Yohana 12:1-19 NEN
Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alikwenda Bethania mahali ambako Lazaro aliyekuwa amefufuliwa na Yesu alikuwa anaishi. Wakaandaa karamu kwa heshima ya Yesu. Martha akawahudumia wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Yesu. Kisha Maria akachukua chupa ya painti moja yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa, akayamimina miguuni mwa Yesu na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato. Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wale wanafunzi ambaye ndiye angemsaliti Yesu, akasema, “Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari 300 na fedha hizo wakapewa maskini?” Yuda alisema hivi si kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwizi, kwani ndiye alikuwa akitunza mfuko wa fedha akawa anaiba kile kilichowekwa humo. Yesu akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu. Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.” Umati mkubwa wa Wayahudi walipojua kwamba Yesu alikuwa huko Bethania, walikuja si tu kwa ajili ya Yesu, lakini pia kumwona Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua. Kwa hiyo viongozi wa makuhani wakafanya mpango wa kumuua Lazaro pia, kwa kuwa kutokana na habari za kufufuliwa kwake Wayahudi wengi walikuwa wanamwendea Yesu na kumwamini. Siku iliyofuata umati mkubwa uliokuwa umekuja kwenye Sikukuu walisikia kwamba Yesu angekuja Yerusalemu. Basi wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki, huku wakipaza sauti wakisema, “Hosana!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!” “Amebarikiwa Mfalme wa Israeli!” Yesu akamkuta mwana-punda akampanda, kama ilivyoandikwa, “Usiogope, Ewe binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda!” Wanafunzi wake Yesu mwanzoni hawakuelewa mambo haya, lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka kuwa mambo haya yalikuwa yameandikwa kwa ajili yake na alitendewa yeye. Wale waliokuwepo wakati Yesu alipomwita Lazaro kutoka kaburini na kumfufua kutoka kwa wafu, waliendelea kushuhudia. Ni kwa sababu pia walikuwa wamesikia kwamba alikuwa ametenda muujiza huu ndiyo maana umati wa watu ukaenda kumlaki. Hivyo Mafarisayo walipoona hayo wakaambiana, “Mnaona, hamwezi kufanya lolote. Angalieni, ulimwengu wote unamfuata yeye!”