Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 11:1-27

Yohane 11:1-27 BHN

Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake. Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa). Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: “Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!” Yesu aliposikia hivyo, akasema, “Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe.” Yesu aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro. Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi. Kisha akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni tena Yudea!” Wanafunzi wakamwambia, “Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?” Yesu akajibu, “Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu. Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake.” Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, ikiwa amelala, basi atapona.” Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro. Basi, Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa; lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni kwake.” Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, “Twendeni nasi tukafe pamoja naye!” Yesu alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne. Kijiji cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu, umbali upatao kilomita tatu. Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha kaka yao. Basi, Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini Maria alibaki nyumbani. Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa! Lakini najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.” Yesu akamwambia, “Kaka yako atafufuka.” Martha akamjibu, “Najua kwamba atafufuka wakati wa ufufuo, siku ya mwisho.” Yesu akamwambia, “Mimi ndimi ufufuo na uhai. Anayeniamini mimi hata kama anakufa, ataishi; na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe. Je, waamini hayo?” Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana! Mimi naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yohane 11:1-27