Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia UTANGULIZI

UTANGULIZI
Nabii Yeremia aliishi na kufanya huduma yake ya kinabii mwishoni mwa karne ya saba na sehemu ya mwanzo ya karne ya sita K.K., yaani mpaka miaka michache kabla ya watu wa Yuda kupelekwa uhamishoni, mwaka 586. Licha ya mahubiri ya Yeremia, kitabu hiki kinazo pia habari kuhusu mwito wake na mikasa mbalimbali iliyomsibu katika kazi yake. Yeremia alizaliwa katika jamaa ya makuhani, akaitwa na Mungu akiwa bado kijana ili awe msemaji wake, yaani nabii. Alikuwa mtu mtulivu ambaye aliwakabili wafalme, makuhani na manabii wengine wa uongo na hata taifa lote la Israeli, akawadhihirishia na kusisitiza kwamba kuwapinga Wakaldayo waliojiweka tayari kuivamia nchi yao ni kujisumbua bure dhidi ya matakwa ya Mwenyezi-Mungu. Kwa ajili hiyo hawakumpenda na mara nyingi aliponea chupuchupu kuuawa.
Yeremia aliwahakikishia kwamba hekalu la Yerusalemu lingeharibiwa na watu wangechukuliwa uhamishoni kule Babuloni. Walimchukua hadi Misri, ikafikiriwa kuwa huo ungekuwa mwisho wake. Lakini ujumbe wake bado ulikuwa motomoto. Anakumbukwa sana kuhusu maneno yake juu ya Agano Jipya (31:31-34) maneno ambayo yanatumika katika sehemu ya pili ya Biblia, yaani Agano Jipya ambalo lamhusu Yesu Kristo, mpatanishi wa Mungu na binadamu (Ebr 8:8-12).
Sehemu zifuatavyo zaweza kutambuliwa katika kitabu hiki:
Sura 1–25. Sehemu hii inazo habari nyingi juu ya Yeremia mwenyewe; wito wake, huduma yake kama nabii, na mikasa yake nyakati za mfalme Yosia, mfalme Yoakini na mfalme Sedekia.
Sura 26–45. Sehemu hii yahusu mambo aliyosema Yeremia na kufanya miaka ya mwishomwisho, kabla ya utawala wa Yuda kuangamizwa. Wataalamu wa Maandiko Matakatifu wanafikiri mengi ya mambo yanayosemwa hapa yaliandikwa na karani, rafiki yake Yeremia, yaani Baruku.
Sura 46–51. Kama vile katika kitabu cha Isaya, kadhalika na katika Yeremia, kuna mkusanyiko wa makaripio na maonyo dhidi ya mataifa mengine: Misri, Filistia, Moabu, Amoni, Edomu, Damasko, Arabia, Elamu na Babuloni.
Sura 52. Kitabu kinaishia na habari ya kihistoria. Hapa yanasimuliwa matukio yaliyoambatana na kutekwa kwa mji wa Yerusalemu na watu kuchukuliwa uhamishoni Babuloni (taz 2 Wafalme 24:18–25:30).

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia UTANGULIZI: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha