Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waamuzi 10

10
Tola
1Baada ya kifo cha Abimeleki, Tola mwana wa Pua mwana wa Dodo, wa kabila la Isakari, akatokea kuwakomboa Waisraeli. Tola aliishi Shamiri katika nchi ya milima ya Efraimu. 2Alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini na mitatu, kisha akafariki na kuzikwa huko Shamiri.
Yairi
3Baada ya Tola, alitokea Yairi wa Gileadi, akawa mwamuzi wa Waisraeli kwa miaka ishirini na miwili. 4Yairi alikuwa na watoto wa kiume thelathini ambao walipanda punda thelathini na walikuwa na miji thelathini katika nchi ya Gileadi, ambayo mpaka leo inaitwa Hawoth-yairi.#10:4 Hawoth-yairi: Maana yake ni vijiji vya Yairi. 5Yairi alifariki na kuzikwa huko Kamoni.
Yeftha
6Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu wakatumikia Mabaali, Maashtarothi, na miungu ya Shamu, ya Sidoni, ya Moabu, ya Amoni na ya Wafilisti. Walimwacha Mwenyezi-Mungu na wala hawakumwabudu tena. 7Hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa Wafilisti na Waamoni. 8Kwa miaka kumi na minane hao waliwatesa na kuwakandamiza Waisraeli walioishi huko Gileadi katika eneo la Waamori mashariki ya mto Yordani. 9Waamoni nao walivuka mto Yordani kupigana na makabila ya Yuda, Benyamini na Efraimu. Nao Waisraeli wakapata taabu sana.
10Basi wakamlilia Mwenyezi-Mungu, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi yako, maana tumekuacha wewe Mungu wetu, tukatumikia Mabaali.” 11Naye Mwenyezi-Mungu akawaambia, “Je, mimi sikuwakomboa kutoka kwa Wamisri, Waamoni, Waamori, Wafilisti? 12Wasidoni, Waamaleki na Wamidiani waliwakandamiza nanyi mkanililia, nami nikawakomboa mikononi mwao. 13Hata hivyo nyinyi mmeniacha, mkatumikia miungu mingine. Kwa hiyo sitawakomboeni tena. 14Nendeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua. Iacheni hiyo iwakomboe katika taabu zenu!”
15Lakini Waisraeli wakamwambia Mwenyezi-Mungu, “Tumetenda dhambi. Tufanye upendavyo, lakini tunakuomba utuokoe leo.” 16Kisha wakaitupilia mbali miungu ya kigeni, wakamtumikia tena Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu hakuweza kuvumilia zaidi kuona taabu za Waisraeli.
17Waamoni wakajikusanya wakapiga kambi yao huko Gileadi. Waisraeli nao wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Mizpa. 18Waisraeli na viongozi wao wakaulizana, “Ni nani atakayeanza kupigana na Waamoni? Atakayefanya hivyo ndiye atakayekuwa kiongozi wa wakazi wote wa Gileadi.”

Iliyochaguliwa sasa

Waamuzi 10: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia