Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 58:1-10

Isaya 58:1-10 BHN

Mwenyezi-Mungu asema: “Piga kelele, wala usijizuie; paza sauti yako kama tarumbeta. Watangazie watu wangu makosa yao, waambie wazawa wa Yakobo dhambi zao. Siku hata siku wananijia kuniabudu, wanatamani kujua mwongozo wangu, kana kwamba wao ni taifa litendalo haki, taifa lisilosahau sheria za Mungu wao. Wananitaka niamue kwa haki, na kutamani kukaa karibu na Mungu. “Nyinyi mnaniuliza: ‘Mbona tunafunga lakini wewe huoni? Mbona tunajinyenyekesha, lakini wewe hujali?’ “Ukweli ni kwamba wakati mnapofunga, mnatafuta tu furaha yenu wenyewe, na kuwakandamiza wafanyakazi wenu! Mnafunga, na kugombana na kupigana ngumi. Mkifunga namna hiyo maombi yenu hayatafika kwangu juu. Mfungapo, nyinyi mnajitaabisha; mnaviinamisha vichwa vyenu kama unyasi, na kulalia nguo za magunia na majivu. Je, huo ndio mnaouita mfungo? Je, hiyo ni siku inayokubaliwa nami? “La! Mfungo ninaotaka mimi ni huu: Kuwafungulia waliofungwa bila haki, kuziondoa kamba za utumwa, kuwaachia huru wanaokandamizwa, na kuvunjilia mbali udhalimu wote! Mfungo wa kweli ni kuwagawia wenye njaa chakula chako, kuwakaribisha nyumbani kwako maskini wasio na makao, kuwavalisha wasio na nguo, bila kusahau kuwasaidia jamaa zenu. “Mkifanya hivyo mtangara kama pambazuko, mkiwa wagonjwa mtapona haraka. Matendo yenu mema yatawatangulia, nami nitawalindeni kutoka nyuma kwa utukufu wangu. Ndipo mtakapoomba, nami Mwenyezi-Mungu nitawaitikia; mtalia kwa sauti kuomba msaada, nami nitajibu, ‘Niko hapa!’ “Kama mkiiondoa dhuluma kati yenu, mkiacha kudharau wengine na kusema maovu, mkiwapa chakula kwa ukarimu wenye njaa, mkitosheleza mahitaji ya wenye dhiki, mwanga utawaangazia nyakati za giza, giza lenu litakuwa kama mchana.

Soma Isaya 58

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha