Isaya 52:7-15
Isaya 52:7-15 BHN
Tazama inavyopendeza kumwona mjumbe akitokea mlimani, ambaye anatangaza amani, ambaye analeta habari njema, na kutangaza ukombozi! Anauambia mji wa Siyoni: “Mungu wako anatawala!” Sikiliza sauti ya walinzi wako; wanaimba pamoja kwa furaha, maana wanaona kwa macho yao wenyewe, kurudi kwa Mwenyezi-Mungu mjini Siyoni. Pazeni sauti za shangwe, enyi magofu ya Yerusalemu! Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake, ameukomboa mji wa Yerusalemu. Mwenyezi-Mungu ameonesha nguvu yake tukufu, mbele ya mataifa yote. Atawaokoa watu wake, na ulimwengu wote utashuhudia. Ondokeni! Ondokeni! Tokeni hapa; msiguse kitu chochote najisi! Ondokeni huku Babuloni! Jitakaseni enyi mbebao vyombo vya Mwenyezi-Mungu. Safari hii hamtatoka kwa haraka, wala hamtaondoka mbiombio! Maana Mwenyezi-Mungu atawatangulieni, Mungu wa Israeli atawalinda kutoka nyuma. Mungu asema hivi: “Mtumishi wangu atafanikiwa; atatukuzwa na kupewa cheo, atapata heshima kuu. Wengi waliomwona walishtuka, kwa vile sura yake ilikuwa imeharibiwa; hakuwa tena na umbo la kibinadamu! Lakini sasa ameyashangaza mataifa mengi. Wafalme wanaduwaa kwa sababu yake, maana wataona mambo ambayo hawajapata kuambiwa, na kufahamu mambo ambayo hawajapata kusikia.”