Isaya 52:7-15
Isaya 52:7-15 SRUV
Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki! Sauti ya walinzi wako! Wanapaza sauti zao, wanaimba pamoja; Maana wataona jicho kwa jicho, Jinsi BWANA arejeavyo Sayuni. Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, Enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa; Kwa kuwa BWANA amewafariji watu wake, Ameukomboa Yerusalemu. BWANA ameweka wazi mkono wake mtakatifu Machoni pa mataifa yote; Na ncha zote za dunia Zitauona wokovu wa Mungu wetu. Nendeni zenu, nendeni zenu, tokeni huko, msiguse kitu kichafu; tokeni kati yake; iweni safi ninyi mnaochukua vyombo vya BWANA. Maana hamtatoka kwa haraka, wala hamtakwenda kwa kukimbia, kwa sababu BWANA atawatangulia; na Mungu wa Israeli atawafuata nyuma; awalinde. Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa, na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana. Kama vile wengi walivyokustaajabia, (uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu yeyote, na umbo lake zaidi ya wanadamu), ndivyo atakavyowastusha mataifa mengi; wafalme watamfumbia vinywa vyao; maana mambo wasiyoambiwa watayaona; na mambo wasiyoyasikia watayafahamu.