Isaya 52:1-12
Isaya 52:1-12 BHN
Amka! Amka! Jipe nguvu zako ewe mji wa Siyoni! Jivike mavazi yako mazuri, ewe Yerusalemu, mji mtakatifu. Maana hawataingia tena kwako watu wasiotahiriwa na walio najisi. Jikungute mavumbi, uinuke ewe Yerusalemu uliyetekwa nyara! Jifungue minyororo yako shingoni, ewe binti Siyoni uliyechukuliwa mateka. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nyinyi mliuzwa utumwani bila malipo yoyote, na mtakombolewa bila kulipa hata senti moja. Tena mwanzoni nyinyi watu wangu mlikimbilia Misri mkakaa huko. Halafu baadaye Waashuru waliwakandamiza bila sababu yoyote. Katika hali ya sasa napata faida gani kuwaona watu wangu wamepelekwa utumwani? Hao wanaowatawala wanajitapa. Nalo jina langu laendelea kudharauliwa kila siku. Kwa hiyo watu wangu watajua mimi ni nani; siku hiyo watajua kwamba ni mimi ninayesema: Niko!” Tazama inavyopendeza kumwona mjumbe akitokea mlimani, ambaye anatangaza amani, ambaye analeta habari njema, na kutangaza ukombozi! Anauambia mji wa Siyoni: “Mungu wako anatawala!” Sikiliza sauti ya walinzi wako; wanaimba pamoja kwa furaha, maana wanaona kwa macho yao wenyewe, kurudi kwa Mwenyezi-Mungu mjini Siyoni. Pazeni sauti za shangwe, enyi magofu ya Yerusalemu! Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake, ameukomboa mji wa Yerusalemu. Mwenyezi-Mungu ameonesha nguvu yake tukufu, mbele ya mataifa yote. Atawaokoa watu wake, na ulimwengu wote utashuhudia. Ondokeni! Ondokeni! Tokeni hapa; msiguse kitu chochote najisi! Ondokeni huku Babuloni! Jitakaseni enyi mbebao vyombo vya Mwenyezi-Mungu. Safari hii hamtatoka kwa haraka, wala hamtaondoka mbiombio! Maana Mwenyezi-Mungu atawatangulieni, Mungu wa Israeli atawalinda kutoka nyuma.