Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 27

27
1 #27:1 Taz Yobu 41:1; Zab 74:14; 104:26 Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu atautwaa upanga wake mkubwa, mkali na imara, na kuliadhibu dude Lewiyathani#27:1 Lewiyathani: Joka la kutisha katika hadithi za kale, hapa latumiwa kutajia mataifa yaliyokandamiza Israeli. joka lirukalo na danganyifu; Mwenyezi-Mungu ataliua joka liishilo baharini.
2Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu atasema hivi:
“Imbeni utenzi wa shamba langu zuri la mizabibu!#27:2 shamba la mizabibu: Mfano wa Waisraeli, watu wa Mungu.
3Mimi, Mwenyezi-Mungu, ni mkulima wake;
nalimwagilia maji kila wakati,
ninalilinda usiku na mchana,
lisije likaharibiwa na mtu yeyote.
4Silikasirikii tena shamba hili;
kama miiba na mbigili ingelilivamia,
mimi ningepambana nayo na kuichoma moto.
5Maadui za watu wangu wakitaka ulinzi wangu,
basi, na wafanye amani nami;
naam, wafanye amani nami.”
6Itakuja siku wazawa wa Yakobo watashika mizizi;
naam, watu wa Israeli watachanua na kuchipua,
na kuijaza dunia yote kwa matunda.
7Mungu hakuwaadhibu Waisraeli vikali
kama alivyowaadhibu maadui wake;
Waisraeli waliopotea vitani,
ni wachache kuliko wale wa maadui zake.
8Aliwaadhibu watu wake kwa kuwapeleka uhamishoni.
Wakati wa upepo mkali wa mashariki,
aliwaondoa kwa kipigo kikali.
9Hivi ndivyo uovu wa wazawa wa Yakobo utakavyoondolewa,
hivi ndivyo dhambi yake itakavyofutwa kabisa:
Ataziharibu madhabahu za miungu;
mawe yake yatasagwasagwa kama chokaa;
Ashera, wala madhabahu za kufukizia ubani hazitabaki.
10Mji ule wa ngome sasa umekuwa mtupu,
umeachwa na kuhamwa kama jangwa,
humo ndama wanalisha na kupumzika.
11Matawi ya miti yamekauka na kuvunjika;
kina mama huyaokota wakawashia moto.
Watu hawa hawajaelewa kitu,
kwa hiyo Mungu, Muumba wao, hatawahurumia,
yeye aliyewafanya, hatawafadhili.
12Siku hiyo, kutoka mto Eufrate hadi mpakani mwa Misri, Mwenyezi-Mungu ataipura nafaka yake, nanyi Waisraeli mtakusanywa mmojammoja. 13Siku hiyo, tarumbeta kubwa itapigwa na watu wote wa Israeli waliopotea nchini Ashuru au waliotawanywa nchini Misri watarudi na kumwabudu Mwenyezi-Mungu juu ya mlima mtakatifu huko Yerusalemu.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 27: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha