Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 19

19
Mungu ataiadhibu nchi ya Misri
1 #19:1-25 Taz Yer 46:2-26; Eze 29:1--32:32 Kauli ya Mungu dhidi ya nchi ya Misri.
“Mwenyezi-Mungu amepanda juu ya wingu liendalo kasi
na kuja mpaka nchi ya Misri.
Sanamu za miungu ya Wamisri zitatetemeka mbele yake,
mioyo ya Wamisri itayeyuka kwa hofu.
2Mimi nitawachochea Wamisri wagongane:
Ndugu na ndugu yake,
jirani na jirani yake,
mji mmoja na mji mwingine,
mfalme mmoja na mfalme mwingine.
3Nitawaondolea Wamisri uhodari wao,
nitaivuruga mipango yao;
watatafuta maoni kwa sanamu na mizimu,
wachawi, mizuka na pepo.
4Nitawatia Wamisri mikononi mwa bwana katili,
mfalme mkali ambaye atawatawala.
Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nimenena.”
5Maji ya mto Nili yatakaushwa,
nao utakauka kabisa.
6Mifereji yake itatoa uvundo,
vijito vyake vitapunguka na kukauka.
Nyasi na mafunjo yake yataoza.
7Sehemu za kandokando ya Nili zitakuwa tupu.
Mimea yote iliyopandwa humo itakauka
na kupeperushiwa mbali na kutoweka.
8Wavuvi watalia na kuomboleza,
wote watumiao ndoana watalalama;
wote wanaotanda nyavu majini watakufa moyo.
9Wafuma nguo za kitani watakata tamaa,
wote kwa pamoja watakufa moyo.
10Wafuma nguo watafedheheshwa,
na vibarua watahuzunika.
11Viongozi wa mji wa Soani ni wapumbavu kabisa,
washauri wa Farao wanatoa shauri la kijinga!
Awezaje kila mmoja kumwambia Farao,
“Mimi ni mzawa wa mtaalamu stadi;
mzawa wa wafalme wa hapo kale!”
12Wako wapi, ewe Farao, wataalamu wako?
Waache basi wakuambie na kukujulisha
aliyopanga Mwenyezi-Mungu wa majeshi dhidi ya Misri!
13Lakini viongozi wa Soani ni wapumbavu,
wakuu wa Memfisi wamedanganyika.
Hao walio msingi wa makabila yao
wamelipotosha taifa la Misri.
14Mwenyezi-Mungu amewamwagia hali ya vurugu,
wakawapotosha Wamisri katika mipango yao yote,
wakawa kama mlevi anayeyumbayumba akitapika.
15Hakuna mtu yeyote nchini Misri,
kiongozi au raia, mashuhuri au duni,
awezaye kufanya lolote la maana.
Wamisri watamwabudu Mwenyezi-Mungu
16Siku ile watu wa Misri wataogopa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu watakapomwona Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameunyosha mkono wake dhidi yao. 17Yuda atakuwa tishio kubwa kwa Wamisri. Wote watakaoambiwa habari za Yuda wataingiwa na woga kwa sababu ya jambo aliloamua Mwenyezi-Mungu wa majeshi kuwatenda.
18Siku hiyo lugha ya Kiebrania itatumika katika miji mitano ya Misri, na watu wa miji hiyo wataapa kuwa waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Mji mmojawapo utaitwa “Mji wa Jua.”#19:18 Mji wa Jua: Au Heliopoli, mji ulioko katika delta ya mto Nili; tafsiri nyingine: Mji wa Uharibifu.
19Siku hiyo, kutakuwa na madhabahu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu katikati ya nchi ya Misri, na nguzo iliyowekwa wakfu kwa Mungu kwenye mpaka wa Misri. 20Madhabahu hiyo itakuwa ishara na ushuhuda kwake Mwenyezi-Mungu wa majeshi katika nchi ya Misri. Watu wakimlilia Mwenyezi-Mungu humo kwa sababu ya kukandamizwa, yeye atawapelekea mkombozi atakayewatetea na kuwakomboa. 21Mwenyezi-Mungu atajijulisha kwa Wamisri na hapo ndipo Wamisri watakapomkiri na kumwabudu kwa kumtolea tambiko na sadaka za kuteketezwa. Hali kadhalika, watamwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri ambazo watazitimiza. 22Mwenyezi-Mungu atawaadhibu Wamisri na kuwaponya. Nao watamrudia, naye atayasikiliza maombi yao na kuwaponya.
23Wakati huo, kutakuwa na barabara kuu kutoka nchi ya Misri hadi nchi ya Ashuru. Waashuru watawatembelea Wamisri, na Wamisri watawatembelea Waashuru; nao wote watamwabudu Mungu pamoja. 24Wakati huo, Israeli itahesabiwa pamoja na Misri na Ashuru; mataifa haya matatu yatakuwa baraka kwa dunia yote. 25Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawabariki na kusema, “Wabarikiwe Wamisri watu wangu, kadhalika na Waashuru ambao ni ishara ya kazi yangu na Waisraeli walio mali yangu.”

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 19: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha