Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 11:8-19

Waebrania 11:8-19 BHN

Kwa imani Abrahamu alimtii Mungu alipoitwa aende katika nchi ambayo Mungu angempa iwe yake. Ingawa hakujua alikokuwa anakwenda, Abrahamu alihama. Kwa imani aliishi kama mgeni katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Aliishi huko katika hema kama walivyoishi Isaka na Yakobo, ambao pia walishiriki ahadi ileile. Maana Abrahamu alikuwa akingojea mji wenye misingi imara, mji ambao Mungu mwenyewe ndiye fundi aliyeubuni na kuujenga. Kwa imani hata Sara aliamini kwamba Mungu hutimiza ahadi zake, kwa hiyo akajaliwa kuchukua mimba ingawaje alikuwa amepita umri. Kwa hiyo, kutoka katika mtu huyo mmoja, Abrahamu, ambaye alikuwa kama amekufa, walitokea watu wengi wasiohesabika kama vile nyota za mbinguni na mchanga wa pwani. Watu hawa wote walikufa wakiwa na imani. Walikufa kabla ya kupokea mambo ambayo Mungu alikuwa ameahidi, lakini kwa mbali waliyaona, wakashangilia, na kukiri wazi kwamba wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani. Watu wanaosema mambo kama hayo, huonesha wazi kwamba wanaitafuta nchi yao wenyewe. Kama wangalikuwa wanaifikiria nchi walikotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko. Lakini sasa wanataka nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Ndio maana Mungu haoni haya wakimwita yeye Mungu wao, kwa sababu yeye mwenyewe amekwisha watayarishia mji. Kwa imani Abrahamu alimtoa tambiko mwanawe Isaka wakati Mungu alipomjaribu. Huyo Abrahamu ndiye aliyekuwa amepokea ahadi ya Mungu, lakini, hata hivyo, alikubali kumtoa tambiko mwanawe wa pekee, ingawa Mungu alikuwa amemwambia: “Wazawa wako watatokana na Isaka.” Abrahamu aliamini kwamba Mungu anaweza kuwafufua wafu; na kwa namna fulani kweli Abrahamu alimpata tena mwanawe kutoka kwa wafu.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Waebrania 11:8-19

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha