Waebrania 11:7-22
Waebrania 11:7-22 BHN
Kwa imani Noa alionywa na Mungu juu ya mambo ya baadaye ambayo hayakuwa yameonekana bado. Alimtii Mungu, akajenga ile safina ambamo aliokolewa yeye pamoja na jamaa yake. Kutokana na hayo ulimwengu ulihukumiwa, naye Noa akapokea uadilifu unaotokana na imani. Kwa imani Abrahamu alimtii Mungu alipoitwa aende katika nchi ambayo Mungu angempa iwe yake. Ingawa hakujua alikokuwa anakwenda, Abrahamu alihama. Kwa imani aliishi kama mgeni katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Aliishi huko katika hema kama walivyoishi Isaka na Yakobo, ambao pia walishiriki ahadi ileile. Maana Abrahamu alikuwa akingojea mji wenye misingi imara, mji ambao Mungu mwenyewe ndiye fundi aliyeubuni na kuujenga. Kwa imani hata Sara aliamini kwamba Mungu hutimiza ahadi zake, kwa hiyo akajaliwa kuchukua mimba ingawaje alikuwa amepita umri. Kwa hiyo, kutoka katika mtu huyo mmoja, Abrahamu, ambaye alikuwa kama amekufa, walitokea watu wengi wasiohesabika kama vile nyota za mbinguni na mchanga wa pwani. Watu hawa wote walikufa wakiwa na imani. Walikufa kabla ya kupokea mambo ambayo Mungu alikuwa ameahidi, lakini kwa mbali waliyaona, wakashangilia, na kukiri wazi kwamba wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani. Watu wanaosema mambo kama hayo, huonesha wazi kwamba wanaitafuta nchi yao wenyewe. Kama wangalikuwa wanaifikiria nchi walikotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko. Lakini sasa wanataka nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Ndio maana Mungu haoni haya wakimwita yeye Mungu wao, kwa sababu yeye mwenyewe amekwisha watayarishia mji. Kwa imani Abrahamu alimtoa tambiko mwanawe Isaka wakati Mungu alipomjaribu. Huyo Abrahamu ndiye aliyekuwa amepokea ahadi ya Mungu, lakini, hata hivyo, alikubali kumtoa tambiko mwanawe wa pekee, ingawa Mungu alikuwa amemwambia: “Wazawa wako watatokana na Isaka.” Abrahamu aliamini kwamba Mungu anaweza kuwafufua wafu; na kwa namna fulani kweli Abrahamu alimpata tena mwanawe kutoka kwa wafu. Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau, wapate baraka zitakazokuja baadaye. Kwa imani Yakobo alipokuwa karibu kufa, aliwabariki kila mmoja wa wana wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiegemea kichwa cha ile fimbo yake. Kwa imani Yosefu alipokuwa karibu kufa, alinena juu ya kutoka kwa Waisraeli katika nchi ya Misri, na pia akawaachia maagizo kuhusu mifupa yake.