Mwanzo 4:1-9
Mwanzo 4:1-9 BHN
Adamu akalala na Hawa mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, “Nimepata mtoto wa kiume kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu!” Halafu akamzaa Abeli nduguye. Abeli alikuwa mfugaji kondoo na Kaini alikuwa mkulima. Baada ya muda fulani, Kaini alimtolea Mwenyezi-Mungu sadaka kutokana na mazao ya shambani, naye Abeli akamtolea Mungu sadaka ya wazawa wa kwanza wa kondoo wake na nyama nono. Mwenyezi-Mungu akapendezwa na Abeli na tambiko yake, lakini hakupendezwa na Kaini wala na tambiko yake. Basi, Kaini akakasirika sana na uso wake ukakunjamana. Mwenyezi-Mungu akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika, na kwa nini uso wako umekunjamana? Je, ukitenda vyema hutakubaliwa? Na usipotenda vyema, basi, dhambi inakuvizia mlangoni; inakutamani, lakini unapaswa kuishinda.” Baadaye, Kaini akamwambia Abeli nduguye, “Twende nje shambani” Basi, walipokuwa shambani, Kaini akamvamia Abeli nduguye, akamuua. Mwenyezi-Mungu akamwuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Kaini akamjibu, “Mimi sijui! Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”