Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 3:1-12

Mwanzo 3:1-12 BHN

Nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini walioumbwa na Mwenyezi-Mungu. Basi, nyoka akamwambia huyo mwanamke, “Ati Mungu alisema msile matunda ya mti wowote bustanini?” Mwanamke akamjibu huyo nyoka, “Twaweza kula matunda ya mti wowote bustanini; lakini Mungu alisema, ‘Msile matunda ya mti ulio katikati ya bustani, wala msiuguse, msije mkafa.’” Nyoka akamwambia mwanamke, “Hamtakufa! Mungu alisema hivyo kwa sababu anajua kwamba mkila matunda ya mti huo mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Basi, mwanamke alipoona kuwa mti huo ni mzuri kwa chakula, wavutia macho, na kwamba wafaa kwa kupata hekima, akachuma tunda lake, akala, akampa na mumewe, naye pia akala. Mara macho yao yakafumbuliwa, wakatambua kwamba wako uchi; hivyo wakajishonea majani ya mtini, wakajifanyia mavazi ya kiunoni. Jioni, wakati wa kupunga upepo, huyo mwanamume na mkewe wakasikia hatua za Mwenyezi-Mungu akitembea bustanini, nao wakajificha kati ya miti ya bustani, Mwenyezi-Mungu asipate kuwaona. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwita huyo mwanamume, “Uko wapi?” Naye akamjibu, “Nimesikia hatua zako bustanini, nikaogopa na kujificha, maana nilikuwa uchi.” Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Nani aliyekuambia kwamba uko uchi? Je, umekula tunda la mti nililokuamuru usile?” Huyo mwanamume akajibu, “Mwanamke uliyenipa akae pamoja nami ndiye aliyenipa tunda la mti huo, nami nikala.”

Soma Mwanzo 3

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 3:1-12