Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 29:13-30

Mwanzo 29:13-30 BHN

Labani aliposikia habari za Yakobo, mpwa wake, alikwenda mbio kumlaki, akamkumbatia, akambusu, akamkaribisha nyumbani kwake. Yakobo akamsimulia Labani mambo yote yaliyotokea. Naye Labani akasema, “Hakika, wewe ni jamaa yangu, damu moja nami!” Yakobo akakaa naye kwa muda wa mwezi mmoja. Siku moja Labani alimwambia Yakobo, “Wewe ni jamaa yangu lakini hiyo haimaanishi kwamba utanitumikia bure. Niambie unataka ujira kiasi gani!” Sasa, Labani alikuwa na binti wawili: Mkubwa aliitwa Lea, na mdogo aliitwa Raheli. Lea alikuwa na macho dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo na wa kupendeza. Yakobo alimpenda Raheli; kwa hiyo akamwambia Labani, “Nitakutumikia miaka saba ili unioze Raheli, binti yako mdogo.” Labani akamwambia, “Afadhali nimwoze Raheli kwako wewe kuliko kumwoza mtu mwingine yeyote. Endelea kuishi nami.” Basi, Yakobo akamtumikia Labani miaka saba kwa ajili ya Raheli, lakini kwake muda huo ulikuwa kama siku chache, kwa vile alivyompenda Raheli. Kisha Yakobo akamwambia Labani, “Muda wangu umetimia, kwa hiyo nipe mke wangu.” Basi, Labani akaandaa karamu na kuwaalika watu wote wa huko. Lakini jioni, Labani akamchukua Lea, binti yake mkubwa, na kumpeleka kwa Yakobo. Yakobo akalala naye. (Labani akamtoa Zilpa, mjakazi wake, awe mtumishi wa Lea.) Asubuhi, Yakobo akagundua ya kuwa ni Lea! Basi, akamwuliza Labani, “Umenitendea jambo gani? Je, si nilikutumikia kwa ajili ya Raheli? Mbona basi, umenidanganya?” Labani akamjibu, “Nchini mwetu hatufanyi hivyo; si desturi yetu kumwoza binti mdogo kabla ya mkubwa. Mtimizie Lea siku zake saba, nasi tutakupa Raheli kwa utumishi wa miaka saba mingine.” Yakobo akakubali. Na Yakobo alipomtimizia Lea siku zake saba, Labani akampa Raheli, binti yake mdogo awe mke wake. (Labani akamtoa Bilha, mjakazi wake, awe mtumishi wa Raheli). Basi, Yakobo akalala na Raheli pia. Lakini Yakobo akampenda Raheli kuliko Lea; akamtumikia Labani miaka mingine saba.

Soma Mwanzo 29

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 29:13-30

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha