Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 46:16-24

Ezekieli 46:16-24 BHN

“Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ikiwa mtawala anampa mmojawapo wa wanawe zawadi ya ardhi, zawadi hiyo itakuwa mali ya huyo kijana milele kama sehemu ya jamaa yake. Lakini ikiwa atampa mmoja wa watumishi wake sehemu yoyote ya ardhi yake, zawadi hiyo itakuwa mali yake mpaka mwaka wa kuachwa huru. Ndipo itakapomrudia mtawala. Ni yeye tu na watoto wake wa kiume wanaoweza kuimiliki daima. Mtawala kamwe asipore mali ya watu. Ardhi yoyote anayowapa watoto wake wa kiume ni lazima itokane na eneo lake mwenyewe. Hivyo hatawadhulumu watu wangu kwa kuwanyanganya ardhi yao.” Kisha, yule mtu akanipitisha kwenye nafasi ya kupitia kuingia kwenye vyumba vitakatifu vya makuhani vinavyoelekea kaskazini, karibu na lango la kusini la ukumbi wa ndani. Akanionesha mahali, upande wa magharibi wa vyumba, akaniambia: “Hapa makuhani huchemsha nyama ya sadaka ya kuondoa hatia, sadaka ya kuondoa dhambi, na kuoka sadaka za nafaka. Kwa hiyo hawatoki nje ya ukumbi na chochote, ili watu wasije wakawa najisi kwa kugusa kitu kitakatifu.” Kisha akanipeleka kwenye uwanja wa nje, akanipitisha karibu na pembe nne za ua; kwa kila pembe ya ua kulikuwapo kiwanja kidogo, yaani, kwa pembe nne za ua vilikuwapo viwanja vinne vidogo vya urefu wa mita 20 na upana mita 15. Ulikuwapo ukuta kukizunguka kila kiwanja, na mahali pa moto mkabala na ukuta. Yule mtu akaniambia: “Haya ni majiko ambako watumishi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu watachemsha sadaka wanazoleta watu.”