Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 35

35
Unabii juu ya Edomu
1Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu! Ugeukie mlima Seiri, utoe unabii juu ya wakazi wake. 3Uambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi napambana nawe, ee mlima Seiri. Ninanyosha mkono wangu dhidi yako na kukufanya uwe jangwa na ukiwa. 4Ninaifanya miji yako kuwa magofu nawe utakuwa jangwa. Ndipo utakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. 5Ulikuwa adui wa daima wa Israeli, ukasababisha watu wake wauawe kwa upanga, wakati wa msiba wao, wakati wa adhabu yao ya mwisho. 6Kwa hiyo, kama niishivyo, nasema mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, naapa kwamba kifo kinakungoja na hutaweza kukikwepa. Kwa kuwa unayo hatia ya mauaji, basi mauaji nayo yatakuandama. 7Nitaufanya mlima Seiri kuwa ukiwa na jangwa na yeyote apitaye huko nitamwangamiza. 8Nitajaza milima yako watu waliouawa; na katika vilima vyako na mabonde yako na magenge yako yote watakuwako waliouawa kwa upanga. 9Nitakufanya kuwa jangwa milele, na miji yako haitakaliwa tena. Ndipo utatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
10“Wewe ulisema ya kwamba mataifa hayo mawili yaani Yuda na Israeli ni mali yako na kwamba utazimiliki! Ulisema hivyo ingawa humo ni makao yangu mimi Mwenyezi-Mungu. 11Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu naapa kwa nafsi yangu kwamba nitakutenda kadiri ya hasira na wivu wako, kulingana na chuki yako kwao. Nitakapokuadhibu utatambua mimi ni nani! 12Wewe utajua ya kwamba mimi mwenyewe Mwenyezi-Mungu nimeyasikia matusi yote uliyoyatoa dhidi ya milima ya Israeli, ukisema: ‘Milima ya Israeli imefanywa kuwa jangwa! Tumepewa sisi tuinyakue!’ 13Nimesikia jinsi unavyojigamba na kusema maneno mengi dhidi yangu. 14Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitakapokufanya wewe Edomu kuwa jangwa, dunia yote itafurahi 15kama wewe ulivyofanya wakati nchi ya Waisraeli ilipoharibiwa. Utakuwa jangwa, ewe mlima Seiri, pamoja na nchi yote ya Edomu. Ndipo watu watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 35: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha