Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka UTANGULIZI

UTANGULIZI
Kitabu cha Kutoka ni kitabu cha pili katika orodha ya vitabu vya Agano la Kale, cha kwanza kikiwa Kitabu cha Mwanzo. Maneno “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri ambako mlikuwa watumwa” (Sura 20:20), yanagusia jambo muhimu la kitabu hiki: Mungu ndiye mkombozi wa watu wake.
Jina la kitabu hiki KUTOKA ni tafsiri ya jina la Kigiriki “eksodos” ambalo lahusu tukio maalumu kabisa katika historia ya Waisraeli: Kutolewa kwao utumwani Misri, kuvuka bahari ya Shamu na safari yao jangwani hadi mlima Sinai.
Kule mlimani Sinai, Mungu alijijulisha kwao, akaratibisha uhusiano wake nao kwa kuwawekea agano lake na mwongozo utakaoimarisha uhusiano huo, yaani amri kumi na maagizo mengine kuhusu namna ya kuishi.
Mhusika mkuu katika kitabu hiki ni Mose. Mose aliitwa na Mungu kuwaongoza Waisraeli kutoka Misri. Yeye anaonekana katika kitabu hiki kuwa msemaji wa Mungu kwa watu wa Israeli. Aliwaongoza safarini kwa niaba ya Mungu na kuwajulisha matakwa ya Mungu.
Kitabu hiki chagawanyika katika sehemu tano:
Sura 1-18 Kukombolewa utumwani Misri na safari mpaka mlima Sinai. Katika sehemu hii tunahabarishwa juu ya kukandamizwa kwa Waisraeli kule Misri, halafu kwa mara ya kwanza Mose anatajwa, naye ni wa ukoo wa Lawi. Mungu alijijulisha kwa Mose kama MIMI NDIMI NILIYE msemo ambao huenda ndio ulio kiini cha jina “Yahweh” ambalo katika tafsiri hii ni Mwenyezi-Mungu. Mungu alimkabidhi Mose jukumu la kumwambia mfalme (Farao) wa Misri kuwaachia Waisraeli waondoke. Farao akakataa na hapo tunasimuliwa juu ya mapigo kumi na kuondoka kwa Waisraeli. Hatimaye tunahabarishwa juu ya kuanzishwa kwa sikukuu ya Pasaka, juu ya kuvuka bahari ya Shamu na kuwasili katika jangwa la Sinai.
Sura 19-24 Kukutana kwa Mungu na Waisraeli na kuratibishwa kwa uhusiano kati yake na wao. Katika sehemu hii Waisraeli wanapewa mwongozo wa maisha, amri kumi na maagizo kadha wa kadha kuhusu maisha ya kawaida na ya ibada. Kisha tunajulishwa jinsi agano kati ya Mungu na watu hao lilivyofanywa. Ilani kuu wanayopewa, ilani ambayo itakuwa ni mwongozo wa maisha ya kidini ya Waisraeli ni hii: “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekutoa nchini Misri ambako ulikuwa mtumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi.” (20:2-3).
Sura 25-31 Katika sehemu hii tunaelezwa jinsi Mose alivyoagizwa na Mungu kutengeneza hema takatifu (hema la mkutano) na sanduku la agano.
Sura 32-34 Sehemu hii aghalabu yahusika na uasi wa Waisraeli walipojitengenezea sanamu ya ndama na kuiabudu wakati Mose alipokuwa amekwenda kuzungumza na Mungu mlimani Sinai (Hapo awali Mose alikuwa amewaambia wazi wazi kwamba Mungu hawezi kufananishwa na kiumbe chochote.)
Sura 36-40 Hapa tunahabarishwa zaidi juu ya hema takatifu na kuwekwa wakfu kwake. Katika hema hilo Mungu alikutana mara kwa mara na Mose.
Kwa jumla, kitabu hiki chatuonesha hasa juu ya uhuru wa kweli, uhuru ambao Mungu anawapatia watu wake wapate kuwa na uhusiano mwema naye, na baina yao wenyewe.

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka UTANGULIZI: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia