Kutoka 5:1-18
Kutoka 5:1-18 BHN
Baadaye, Mose na Aroni walimwendea Farao, wakamwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli anasema hivi, ‘Waache watu wangu waondoke, wakanifanyie sikukuu jangwani.’” Lakini Farao akawauliza, “Ni nani huyo Mwenyezi-Mungu, hata nimsikilize na kuwaacha Waisraeli waondoke? Mimi simtambui huyo Mwenyezi-Mungu, wala sitawaruhusu Waisraeli waondoke.” Mose na Aroni wakamwambia, “Mungu wa Waebrania amekutana nasi. Tunakusihi utuache twende zetu jangwani mwendo wa siku tatu tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. La sivyo, yeye atatuua kwa maradhi mabaya au vita.” Lakini mfalme wa Misri akawajibu, “Enyi Mose na Aroni, kwa nini mnajaribu kuwatoa watu kazini mwao? Rudini kazini mwenu.” Tena Farao akasema, “Hawa watu wenu ni wengi kuliko wananchi; mnataka waache kufanya kazi!” Siku hiyohiyo Farao aliwaamuru wanyapara pamoja na wasimamizi, akasema, “Tangu leo msiwape watu hawa nyasi za kutengenezea matofali kama ilivyo kawaida. Wao wenyewe watakwenda kujitafutia. Lakini idadi ya matofali yanayotengenezwa kila siku iwe ileile, wala lisipungue hata tofali moja, kwa kuwa watu hawa ni wavivu ndio maana wanapiga kelele: ‘Tuache twende tukamtambikie Mungu wetu.’ Wazidishieni watu hawa kazi ngumu ili waitolee jasho na kuacha kusema maneno ya uongo.” Basi, wanyapara na wasimamizi wa watu wakatoka na kuwaambia watu, “Farao anasema hivi, ‘Sitawapeni nyasi. Nendeni nyinyi wenyewe mkatafute popote mtakapoweza kuzipata, na wala kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’” Basi, watu wote wakatawanyika kila mahali nchini Misri wakitafuta nyasi za kutengenezea matofali. Nao Wanyapara wakakazana wakisema, “Timizeni kazi yenu ya kila siku kama hapo awali mlipoletewa nyasi.” Wanyapara Wamisri wakawapiga wasimamizi wa Waisraeli waliochaguliwa kusimamia kazi wakisema, “Kwa nini hamtimizi kazi yenu na kufikisha idadi ileile ya matofali kama awali?” Ndipo wasimamizi wa Waisraeli walipomwendea Farao, wakamlilia wakisema, “Kwa nini unatutenda hivi sisi watumishi wako? Hatupewi tena nyasi zozote na huku tunalazimishwa kufyatua matofali. Tena sisi watumishi wako tunapigwa, hali kosa ni la watu wako.” Lakini Farao akasema, “Wavivu nyinyi; nyinyi ni wavivu, ndio maana mnasema, ‘Tuache twende tukamtambikie Mwenyezi-Mungu’. Nendeni sasa mkafanye kazi; maana hamtapewa nyasi zozote na mtafyatua idadi ileile ya matofali.”