Kutoka 32:7-14
Kutoka 32:7-14 BHN
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Teremka chini kwa maana watu wako uliowaleta kutoka nchini Misri wamejipotosha wenyewe; wameiacha mara moja njia niliyowaamuru, wakajifanyia ndama wa kusubu, nao wamemwabudu na kumtolea tambiko wakisema, ‘Ee Israeli, huyu ndiye mungu wetu aliyetutoa nchini Misri!’ Nawafahamu watu hawa; wao wana vichwa vigumu. Sasa, usijaribu kunizuia. Niache niwaangamize kwa ghadhabu kali; kisha kutokana nawe nitaunda taifa kubwa.” Lakini Mose akamsihi Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, kwa nini hasira yako inawaka vikali dhidi ya watu wako uliowatoa nchini Misri kwa uwezo mkuu na mkono wenye nguvu? Ukifanya hivyo, hakika Wamisri watasema, ‘Aliwatoa kwa nia mbaya ili kuwaulia mlimani na kuwateketeza kabisa duniani.’ Ee Mwenyezi-Mungu, tuliza hasira yako kali na kuacha jambo hilo baya ulilokusudia kufanya dhidi ya watu wako. Wakumbuke watumishi wako, Abrahamu, Isaka na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe, ukisema, ‘Nitawazidisha wazawa wenu kama nyota za mbinguni na nchi yote hii niliyowaahidia nitawapa vizazi vyenu wairithi milele.’” Basi, Mwenyezi-Mungu akaacha kuwafanyia watu wake lile jambo baya alilokuwa amesema.