Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waefeso 2:11-19

Waefeso 2:11-19 BHN

Nyinyi mlio kwa asili watu wa mataifa mengine – mnaoitwa, “Wasiotahiriwa” na Wayahudi ambao hujiita, “Waliotahiriwa,” (kwa sababu ya kile wanachoifanyia miili yao) – kumbukeni mlivyokuwa zamani. Wakati ule nyinyi mlikuwa bila Kristo; mlikuwa nje ya jamii ya Israeli; mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu katika yale maagano aliyoahidi Mungu. Mlikuwa bila matumaini na kama watu wasiomjua Mungu hapa duniani. Lakini sasa, kwa kuungana na Kristo Yesu, nyinyi ambao hapo awali mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa njia ya damu yake Kristo. Maana Kristo mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja. Kwa mwili wake yeye mwenyewe aliubomoa ule ukuta uliowatenganisha na kuwafanya maadui. Aliiondoa ile sheria pamoja na amri zake na kanuni zake, ili kutokana na jamii hizo mbili aumbe jamii moja mpya katika umoja naye na hivyo kuleta amani. Kwa mwili wake, Kristo aliuangamiza uadui wao; kwa msalaba wake aliziunganisha jamii hizo kuwa moja na kuzipatanisha na Mungu. Basi, Kristo alikuja akahubiri Habari Njema ya amani kwenu nyinyi watu wa mataifa mengine mliokuwa mbali na Mungu, na pia kwa Wayahudi ambao walikuwa karibu na Mungu. Hivyo, kwa njia yake, sisi sote, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, tunaweza kumwendea Baba kwa Roho mmoja. Basi, nyinyi si wageni tena, wala si watu wa nje. Nyinyi ni raia pamoja na watu wa Mungu, na ni watu wa jamaa ya Mungu.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Waefeso 2:11-19