Mhubiri 1:1-17
Mhubiri 1:1-17 BHN
Yafuatayo ni maneno ya Mhubiri mwana wa Daudi, aliyekuwa mfalme huko Yerusalemu. Bure kabisa, bure kabisa, nakuambia mimi Mhubiri! Kila kitu ni bure kabisa! Binadamu hufaidi nini kwa jasho lake lote hapa duniani? Kizazi chapita na kingine chaja, lakini dunia yadumu daima. Jua lachomoza na kutua; laharakisha kwenda machweoni. Upepo wavuma kusini, wazunguka hadi kaskazini. Wavuma na kuvuma tena, warudia mzunguko wake daima. Mito yote hutiririkia baharini, lakini bahari kamwe haijai; huko ambako mito hutiririkia ndiko huko inakotoka tena. Mambo yote husababisha uchovu, uchovu mkubwa usioelezeka. Jicho halichoki kuona, wala sikio kusikia. Yaliyokuwako ndio yatakayokuwako, yaliyotendeka ndio yatakayotendeka; duniani hakuna jambo jipya. Watu husema, “Tazama jambo jipya,” kumbe lilikwisha kuwako zama za kale. Hakuna mtu anayekumbuka ya zamani wala atakayekumbuka yatakayotukia baadaye. Mimi Mhubiri, nilikuwa mfalme wa Israeli, huko Yerusalemu. Nilipania kuchunguza na kutafuta kwa hekima kila kitu kinachotukia duniani. Hiyo ni taabu kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu. Nimeyaona yote yanayofanywa duniani; yote ni bure: Ni sawa na kufukuza upepo! Kilichopindika hakiwezi kunyoshwa, kisichokuwapo hakiwezi kuhesabiwa. Basi, nikatafakari nikisema, “Nimejipatia hekima nyingi zaidi kupita wote waliopata kutawala Yerusalemu kabla yangu. Naam, nina uzoefu wa hekima na maarifa.” Nilipania kubainisha kati ya hekima, wazimu na upumbavu. Lakini niligundua kwamba kufanya hivyo ni sawa na kufukuza upepo.