Kumbukumbu la Sheria 4:25-31
Kumbukumbu la Sheria 4:25-31 BHN
“Mtakapokuwa mmekaa katika nchi hiyo, mkapata watoto na wajukuu na kuwa wazee, kama mkianza kupotoka na kujifanyia sanamu ya kuchonga katika umbo la kitu chochote, mkafanya uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kumkasirisha, basi, mimi leo naziita mbingu na dunia zishuhudie kati yenu; nawaambieni kwamba mara moja mtaangamia kabisa katika nchi ambayo mnaenda kuimiliki huko ngambo ya mto Yordani. Hamtaishi huko muda mrefu, bali mtaangamizwa kabisa. Mwenyezi-Mungu atawatawanya kati ya mataifa mengine, na ni wachache wenu tu watakaosalia huko ambako Mwenyezi-Mungu atawafukuzia. Huko mtaitumikia miungu ya miti na mawe ambayo imetengenezwa kwa mikono ya watu; na ambayo haiwezi kuona, haisikii, haili wala kunusa. Kisha kutoka humohumo nchini mtamtafuta Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nanyi mtampata kama mkimtafuta kwa moyo wote na roho yote. Mambo haya yote yatakapowapata huko baadaye, mkapata taabu, mtamrudia Mwenyezi-Mungu na kumtii. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni Mungu mwenye rehema, hatawaacheni wala kuwaangamiza, wala kusahau agano ambalo alifanya na wazee wenu kwa kiapo.